Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
MATATIZO ya watoto kuzaliwa na vichwa vikubwa au mgongo wazi ambayo hujulikana kitaalamu ‘Neural tube effect’, yanazidi kuongezeka duniani.
Wataalamu wanaeleza kwamba watoto wengi wanaozaliwa na matatizo haya ni wale walio katika ukanda wa kusini mwa jangwa la Sahara.
Inakadiriwa kwamba kila mwaka watoto 300,000 duniani huzaliwa wakiwa na tatizo la kichwa kikubwa au mgongo wazi.
Inaelezwa kuwa tatizo hutokea pale ‘neural tube’ zinaposhindwa kufunga vizuri kabla ya mtoto kuzaliwa.
Hivyo mtoto husika anapozaliwa sehemu yake kubwa ya ubongo huwa inajaa maji na mgongoni wake unakuwa haujafunga vizuri.
CHANZO CHA TATIZO
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), Dk. Othman Kiloloma, anasema tatizo la mtoto kuzaliwa akiwa na kichwa kikubwa au mgongo wazi linahusisha mfumo wa mshipa wa fahamu uitwao ‘central never system’ na wala si la kurithi.
Anasema tatizo la kichwa kikubwa husababishwa na mfumo wa maji unaozunguka ndani ya kichwa kupata hitilafu hali ambayo husababisha maji kwenda kuziba katika mishipa yake na hatimaye kusababisha kichwa kuwa kikubwa.
Anasema wakati mwingine maji huweza kuzalishwa vizuri lakini yanashindwa kunyonywa kama inavyopaswa na matokeo yake husababisha kichwa kuwa kikubwa.
Anasema tatizo la mgongo wazi hutokea pale mgongo unaposhindwa kujikunja na kuweza kuufunika uti wa mgongo wa mtoto akiwa tumboni.
Nini huchochea hali hiyo
Miaka ya nyuma jamii ilichukulia kwamba mwanamke mwenye umri mkubwa zaidi ndiye mwenye uwezekano wa kuzaa mtoto mwenye kasoro mbalimbali za kimaumbile.
Lakini kadiri miaka inavyosonga mbele mambo yamebadilika sasa na wataalamu wamegundua kwamba si mwanamke pekee anayekumbana na hali hiyo bali hata mwanamume.
Daktari Samwel Swai wa taasisi hiyo, anasema wanaume wengi wenye umri mkubwa wa kuanzia miaka 40 na kuendelea huzalisha mbegu zisizokuwa na ubora.
“Kwa kuwa wengi hawazalishi mbegu zenye ubora wana hatari ya kuzalisha watoto wenye kasoro mbalimbali. Miongoni mwa kasoro hizo ni tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi, na kulingana na maisha ya sasa wanajikuta wanatoa mbegu zisizo kuwa na ubora unaotakiwa,” anasema Dk. Swai.
Dk. Swai anasema tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi pia husababishwa na baadhi ya magonjwa ambayo mama huugua wakati wa ujauzito.
“Mama akiugua baadhi ya magonjwa, kwa mfano malaria na akatibiwa isivyotakiwa, lakini pia mjamzito akitumia baadhi ya dawa kama Metacefline bila kufuata ushauri wa daktari humuweka mtoto aliyeko tumboni katika hatari ya kuathirika,” anasema.
Hali ilivyo nchini
Dk. Kiloloma anasema idadi ya watoto wanaozaliwa wakiwa na tatizo la vichwa vikubwa pamoja na mgongo wazi nchini limezidi kuongezeka katika miaka ya hivi karibuni.
“Takwimu zinaonyesha kuwa kila mwaka wanazaliwa watoto 4,000 wenye matatizo haya lakini wanaoletwa hospitalini kupata matibabu ni watoto 600 pekee, bado hatujui hao 3,400 wanapotelea wapi,” anasema.
Anasema pia upo uhusiano kwamba upungufu wa madini ya folic acid husababisha mtoto kuzaliwa akiwa na tatizo la mgongo wazi.
“Virutubishi hivyo hupatikana kwenye mboga za majani na mama hutakiwa kuzitumia kabla hajapata ujauzito kwani tatizo hutokea ndani ya wiki sita za mwanzo za ujauzito,” anasema.
Anasema hata hivyo mtoto akizaliwa na tatizo hilo na akawahi kufikishwa hospitalini hupona kabisa kwa kufanyiwa upasuaji.
“Tatizo la kichwa kikubwa huwa tunafanya upasuaji wa kuhamisha maji kutoka kichwani kwenda tumboni kwa kutumia njia ya kitaalamu ijulikanayo kama ‘Ventriculo Peritoreal Shunt (VPS)’ au njia nyingine ya mfumo wa ‘Endoscopic Third Ventriculostomy (ETV)’.
“Kwa kutumia njia hizo tunafunua shimo ndani ya kichwa na kisha tunaingiza mpira ambao unapita chini ya ngozi kuelekea tumboni. Ukishaingiza tu kichwa kinaanza kupungua taratibu,” anasema.
Gharama
Dk. Kiloloma anasema gharama ya kuweka kifaa cha kusaidia kunyonya maji kichwani huwa ni kati ya Sh 160,000 hadi Sh milioni moja kulingana na ubora wake.
“Lakini kwa kuwa matibabu kwa watoto ni bure huwa tunafanya hivyo. Tunashukuru wapo wafadhili ambao hujitokeza kusaidia vifaa hivyo lakini wakati mwingine inapotokea vimeisha wazazi hulazimika kwenda kununua ili watoto wao watibiwe,” anasema.
Simulizi za wagonjwa
Neema Dickson (28) mkazi wa Muheza mkoani Tanga, ni mama wa watoto wanne ambao alijifungua salama kwa njia ya kawaida.
Hata hivyo mwanawe wa nne ambaye alijifungua mwaka 2008 amegundulika kuwa na tatizo la kichwa kikubwa.
Neema anasema tatizo hilo liligundulika wakati mtoto huyo alipofikisha umri wa miaka miwili baada ya madaktari kumfanyia uchunguzi wa kina.
“Siku hiyo nilimpeleka kliniki kama kawaida, madaktari walipomuangalia kichwani chake walionesha hali ya wasiwasi, walisema kichwa chake kilikuwa kimeonge ona patwa na wasiwasi juu ya mwenendo wa afya yake.
“Siku hiyo nilimpeleka hospitalini kliniki kama kawaida, daktari mmoja alipomuangalia kichwani alisema mwanangu anaonesha kuwa kichwa chake kina tatizo. Akanishauri nimlete hapa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi,” anasema.
Grace Lugasoo (21) mwenye asili ya kimasai, naye yupo hospitalini hapo na mtoto wake aliyezaliwa Agosti 29, mwaka huu.
Grace anasema mwanawe huyo ni uzao wake wa pili na kwamba alizaliwa salama akiwa hana tatizo lolote lakini hivi sasa amekutwa na tatizo la kichwa kikubwa baada ya kufanyiwa uchunguzi.
“Nilijifungua katika Hospitali ya Mkoa Iringa ambako ndipo ninakoishi na familia yangu, jamii iliyonizunguka walianza kushangaa kwa jinsi ambavyo kichwa cha mwanangu kilikuwa kinaongezeka ukubwa.
“Mama yangu ndiye aliyenishauri kuja Dar es Salaam, nashukuru pale Iringa walinipatia rufaa nikaja MOI ambapo nimeambiwa wakati wowote mwanangu atafanyiwa upasuaji kuwekewa kifaa maalumu kitakachosaidia kichwa chake kisiendelee kuongezeka,” anasema.
Mtwara wanalishwa ugoro
Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi wenye Watoto waliozaliwa na Kichwa Kikubwa (ASBAHT), Abdulhakim Bayakub, anasema wamegundua kuwa wazazi wenye watoto walio na vichwa vikubwa mkoani Mtwara wanawalisha ugoro.
“Jamii haina uelewa wa kutosha kwanini watoto wanazaliwa na tatizo la mgongo wazi na lile la kichwa kikubwa, tumekuta wakiwalisha ugoro wakidhani kuwa ndiyo dawa sahihi itakayowaponyesha watoto wao.
“Kwa kuwa ugoro si dawa sahihi matokeo yake watoto wanakufa, pamoja na hao wapo wengine ambao wanawaua kabisa wakiwaona kuwa ni mikosi ndani ya familia, ndoa zimevunjika kisa mama kajifungua mtoto mwenye kichwa kikubwa,” anasema.
Bayakub anasema wapo wazazi wengine ambao huamini kuwa watoto wao wamerogwa na hivyo kuwapeleka kwa waganga badala ya hospitali ili wapatiwe matibabu.
“Tumetembelea mikoa mingi na kujifunza mengi, kubwa ni kwamba jamii bado inahitaji kupewa elimu sahihi kuhusu matatizo haya, watoto wengi wanapoteza maisha,” anasema.
Jitihada za serikali
Dk. Kiloloma anasema virutubisho vya madini ya ‘folic acid’ ambayo humkinga mtoto aliyeko tumboni asipatwe na tatizo la kichwa kikubwa vimeanza kuwekwa katika unga wa ngano.
Anasema hatua hiyo imekuja baada ya Serikali kupitisha sheria inayowataka wazalishaji wa bidhaa hiyo kuongeza madini hayo ili kukabili ongezeko la idadi ya watoto wanaozaliwa na tatizo hilo.
“Madini ya folic acid hupatikana zaidi kwenye matunda na mbogamboga lakini kutokana na ukubwa wa tatizo serikali imeona ni vema kupitisha sheria hiyo na baadhi ya wazalishaji wa unga wa ngano wameanza kuongeza madini hayo.
“Madini haya ni ya muhimu, uhitajika wakati wa uumbaji wa viungo vya mtoto tumboni, huwa yanatengeneza kitu mfano wa ukuta ambao humkinga mtoto kupata tatizo,” anasema.
Anasema watoto wengine hupatwa na tatizo hilo baada ya mjamzito kupata maambukizi ya virusi kama vile rubella (tetekuwanga).
“Mjamzito akipata rubella na asipotibiwa vema virusi vile husafiri na kwenda kumuathiri mtoto aliyepo tumboni, ndiyo maana tunashauri mama anapohisi ni mjamzito awahi kliniki ili aanze kufuatiliwa kwa ukaribu na wataalamu wa afya,” anasema.
Anasema kwa wiki huona watoto wapatao 10 katika kliniki iliyopo hospitalini hapo na kwa mwaka hutibu watoto zaidi ya 500.
“Hii ni namba kubwa, tunataka tuendelee kuipa elimu jamii kwamba mtoto akiwahishwa matibabu anapona kabisa, zamani walikuwa wanafichwa ndani,” alisema
Dk. Kiloloma anasema MOI imekuwa ikifanya matibabu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwamo Taasisi ya GSM Foundation, Duka la Dawa la Nakiete na wengine.
“Hadi sasa kwa kushirikiana na GSM tumeweza kufanikisha matibabu ya watoto zaidi ya 100 katika mikoa 16 ya Tanzania Bara ambapo wametibiwa bure kwa kuwekewa kifaa maalumu kinachosaidia kunyonya maji yaliyoko kichwani,” anasema.
Anasema wale wa Nakiete wamewezesha kupata viti vya matairi vya wagonjwa 15 vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 10.
“Bado tunahitaji ushirikiano zaidi ili tuweze kuokoa maisha ya watoto wengi ambao tunawapoteza, tunahitaji kuwafuatilia kila mara tujue wapi wanakopelekwa na wale tunaowatibu tuhakikishe wanapofikia umri wa kwenda shule wanapelekwa,” anasema.