DERICK MILTON-SIMIYU
MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Festo Dugange amesema wanaume wengi katika mkoa huo, wamekuwa wakitumia majibu wanayopewa wenza wao pindi wanapokwenda kupima maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi kuwa na wao wako salama bila kwenda kupima wenyewe.
Mbali na hilo, Dk. Dugange alisema endapo majibu yakitoka kwa mweza kuwa ana maambukizi ya VVU na akapewa dawa za kufubaza (ARVs), basi na mwanaume anapaswa kutumia dawa hizo hizo.
Alisema hayo juzi wakati wa kikao cha viongozi wa mkoa, wadau wa afya na wajumbe wa bodi ya shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihususha na masuala ya Afya (AGPAHI) kilichokuwa maalumu kujadili utekelezaji wa mradi wa shirika hilo.
Alisema wanaume wengi hawapendi kwenda kupima, wala kuwasindikiza wenza wao kliniki ili wakapime afya.
“Bado tunachangamoto kubwa ya wanaume kuwasindika wake zao kliniki, ukingalia takwimu zetu kasi ya wanaume kupima afya zao bado si kubwa kama wanawake.
“Wanaume wanatumia vipimo vya wake zao kama kipimo chao na wenyewe, mama akienda kupima kliniki akiambiwa hana Ukimwi na mwanaume anaamini hana…akiambiwa anayo maambukizi basi na mwanaume naye anaamini ana maambukizi,”alisema.
Alisema wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii ili wanaume waweze kutambua umuhimu wa kuwasindikiza wenza wao kliniki.
Meneja Mradi wa AGPAHI Mkoa wa Simiyu, Dk. Julius Sipemba alisema wamesaidia kushusha maambukizi kwa asilimia 90 kwa watu wanaotumia dawa za kufubaza makali ya Ukimwi (ARVs).
Alisema wanatoa huduma za VVU na Ukimwi mkoa mzima ambap wana vituo 233 vya kutolea huduma za afya na 73 kati ya hivyo hupata usimamizi wa moja kwa moja kutoka shirika hilo.
“ Wagonjwa wanaopata huduma kwenye vituo 73 ni sawa na asilimia 95 ya wagonjwa wote walioko vituo 233, pia tunaboresha miundombinu kwa kujenga na kukarabati majengo, huduma za maabara kwa kununua madawa na vifaa,” alisema Dk. Sipemba.