Na GLORY MLAY – DAR ES SALAAM
WANARIADHA wa Tanzania wameshindwa kufuzu kwa mashindano ya Dunia huko Doha, Qatar yanayotarajiwa kufanyika mwakani baada ya kufanya vibaya kwenye mbio za Blom Bank Beirut Marathon zilizofanyika juzi, jijini Beirut huko Lebanon.
Tanzania imewasilishwa na wanariadha wawili, Samson Lyimo na Glory Makula, ambao walikwenda huko kwa ufadhili wa Kampuni ya vinywaji baridi ya SBC baada ya kufanya vema kwenye mbio hizo zinazotambuliwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF).
Katika mashindano hayo mshindi ameibuka Medine Armino wa Ethiopia aliyetumia saa 2:29.30 akifuatiwa na Nazret Gebrehiwet wa Eritrea 2:29.30 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Muethiopia, Selamawit Tsegaw saa 2:31.40.
Kwa upande wa wanaume mshindi aliibuka Mohamed El Aaraby kutoka Morocco aliyetumia saa 2:10.41 akifuatiwa na Mganda Felix Chemonges 2:11.54 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Deresa Ulfata wa Ethiopia aliyetumia saa 2:12.31.