24.3 C
Dar es Salaam
Monday, September 16, 2024

Contact us: [email protected]

Wanaokwepa stempu za kielektroniki jela miaka mitatu, faini milioni 50

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wazalishaji na waagizaji wa bidhaa watakaoshindwa kubandika stempu za kodi za kielektroniki watakabiliwa na faini kati ya Sh milioni 5 hadi 50 au kifungo cha miaka mitatu jela.

Kabla ya kuanzishwa kwa stempu za kodi za kielektroniki Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikuwa ikitumia stempu za karatasi hali iliyosababisha kuwapo ugumu katika kudhibiti bidhaa za magendo na kujua kiwango halisi kilichozalishwa cha bidhaa husika.

Akizungumza Mei 29,2024 wakati wa mafunzo kwa wanachama wa Jumuiya ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (Jumikita), Meneja Mradi Stempu za Kodi za Kielektroniki, Abiud Tweve, amesema mfumo huo umesaidia kulinda mapato ya serikali na kuwezesha kupatikana taarifa za uzalishaji kwa wakati.

“Tunafanya maboresho kila siku kuhakikisha tunatimiza matakwa ya walipakodi wetu, tulipoanza mwaka 2019 bei ya stempu ilikuwa kwa Dola lakini hivi sasa inalipwa kwa shilingi…bei imeshuka kwa zaidi ya asilimia 30,” amesema Tweve.

Kwa mujibu wa meneja huyo, hadi kufikia Machi 2024 mfuo huo una wazalishaji na waagizaji 684 kutoka 87 wa awali na kati yao 192 ni kutoka nje na 492 wa ndani.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa TRA, Hudson Kamoga, amesema mafanikio yanayoonekana katika mamlaka hiyo yamechagizwa na vitu vingi ikiwemo utoaji elimu kwa umma uliowezesha kulipa kodi ya hiyari, kuimarika kwa mifumo kulikorahisisha ukusanyaji wa mapato.

Takwimu za TRA zinaonyesha katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan wamekusanya Sh trilioni 24 mwaka 2022/23 kutoka Sh trilioni 18 mwaka 2020/21.

“Watu wamekuwa na uhiyari wa kulipa kodi, ukwepaji kodi umepungua, tutakapofika mwakani mwezi wa nane tutapunguza kwa kiwango kikubwa sana upotevu wa mapato ya serikali,” amesema Kamoga.

Aidha amesema wanayo programu ijulikanayo kama ‘Mlango kwa mlango’ ambapo wamekuwa wakienda kila duka kusikiliza wateja kubaini changamoto zinazowakabili katika masuala ya kodi.

“Inawezekana mlipakodi anafanya biashara hana leseni, TIN (Namba ya Mlipakodi), hatoi risiti kwahiyo tunawekana sawa, tunaomba wafanyabaishara watoe ushirikiano,” amesema Kamoga.

Kaimu mkurugenzi huyo amesema baada ya Bunge kupitisha sheria ya kutoza kodi biashara za mtandaoni Hadi kufikia Februari 2024 wamekusanya Sh trilioni 12.

“Meta (Kampuni inayomiliki mitandao ya Facebook, Instagram na X) wamekuja, Google wanalipa na mitandao mingine mbalimbali, bado kuna ambao wanafanya biashara kwenye mitandao tunaendelea na usajili na kuwatambua,” amesema.

Mwenyekiti wa Jumikita, Shaaban Matwebe, amesema mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea uwezo Waandishi wa habari mitandaoni hatua itakayowezesha kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali.

“Tunaishukuru TRA kwa kuthamini nguvu ya mitandao ya kijamii, naamini kupitia mafunzo haya tutapata uelewa wa kutosha wa masuala yahusuyo kodi na kuelimisha umma ili kuirahisishia serikali kukusanya mapato,” amesema Matwebe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles