Na MWANDISHI WETU,
WATU wanaoishi karibu na barabara kuu huwa wana viwango vya juu vya matatizo ya kiakili, ambayo kitaalamu huitwa Dementia.
Watu wenye Dementia hukabiliwa na tatizo la kutokumbuka mambo pamoja na uwezo wao wa kutumia ubongo kuwa mdogo.
Hisia zao pia hubadilika na kwa muda mrefu wamekuwa wakidhaniwa kuwa ni watu wenye kichaa.
Matokeo ya utafiti uliochapishwa katika Jarida la Lancet unaonyesha kuwa asilimia 11 ya visa vya Dementia ambavyo hutokea katika eneo la hadi mita 50 kutoka kwenye barabara huenda vinatokana na magari.
Watafiti ambao waliwachunguza watu karibu milioni mbili nchini Canada kwa kipindi cha miaka 11 wanasema uchafuzi wa hewa na kelele kutokana na magari huenda vinachangia katika kuathiri ubongo wa wakazi wa maeneo ya aina hiyo.
Wataalamu wa Dementia nchini Uingereza wanasema matokeo ya utafiti huo yana uzito lakini yanahitaji kuchunguzwa zaidi.
Inakadiriwa kwamba watu karibu milioni 50 kote duniani wanakabiliwa na tatizo la ugonjwa wa Dementia.
Hata hivyo, chanzo hasa cha ugonjwa huo hakijabainika.
Utafiti huo uliofanywa katika Mkoa wa Ontario nchini Canada kati ya mwaka 2001 na 2012 uligundua kuwa watu 243,611 wanakabiliwa na matatizo hayo ya akili. Tatizo hilo lilijitokeza zaidi kwa watu walioishi karibu na barabara kuu.
Wakilinganishwa na waliokaa zaidi ya mita 300 kutoka kwa barabara kuu, hatari ya kuugua ugonjwa huo ilikuwa: Asilimia 7 zaidi kwa waliokuwa 50m; asilimia 4 zaidi kati ya 50-100m
Na asilimia mbili zaidi kati ya 101-200m.
Tathmini hiyo inaonyesha kuwa huenda asilimia 7-11 ya visa vya dementia maeneo yaliyo mita 50 karibu na barabara vimesababishwa na magari.
Hata hivyo, watafiti hao walizingatia mambo mengine ambayo huenda yakachangia ugonjwa huo yakiwamo umaskini, unene, viwango vya elimu na uvutaji wa sigara kuhakikisha havikuathiri matokeo.
Dk. Hong Chen kutoka Ontario, ambaye ni mmoja wa watafiti waliohusika, anasema ikizingatiwa kwamba watu wengi wamekuwa wakihamia mijini na barabara na magari kuongezeka, kuna haja ya uchunguzi zaidi kuhusu athari za magari na barabara kama vile uchafuzi wa hewa na kelele.
Wanadokeza kwamba kelele, vumbi, chembe za naitrojeni oksaidi na chembe za mipira kutoka kwa tairi za magari huenda vinachangia kuongezeka kwa ugonjwa wa dementia kwa wanaoishi karibu na barabara kuu.
Hata hivyo, utafiti huo uliongozwa na maeneo ambayo watu wenye dementia wanaishi.
Hauwezi kuthibitisha kwamba barabara ndizo zinazosababisha ugonjwa huo.
Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa BBC