Na KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
WATUHUMIWA sita wanaodaiwa kumuua aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengodo Mvungi, wameachiwa huru na Mahakama Kuu na kushtakiwa upya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Watuhumiwa hao waliachiwa baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuomba kuondoa shtaka hilo mahakamani.
Jamhuri ikiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nasoro Katuga, iliwasilisha maombi hayo mbele ya Jaji Sam Rumanyika.
Baada ya kuachiwa huru, walikamatwa tena na kupelekwa Mahakama ya Kisutu kwa ajili ya kusomewa mashtaka mapya ya mauaji ya Dk. Mvungi.
Washtakiwa hao ni Msigwa Matonya(35), Mianda Mlewa(45), Paulo Mdonondo (35), Longishu Losindo (34), Juma Kangungu (34) na John Mayunga (60).
Akiwasomea mashtaka mapya mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Mmbando, Wakili wa Serikali, Lilian Rwetabura alidai wanashtakiwa walitenda mauaji hayo kwa kukusudia.
Alida washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo Novemba 3 mwaka 2013 maeneo ya Kibwerenge Msakuzi, Â Â Mbezi.
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hivyo walirudishwa rumande hadi Desemba 6 mwaka huu.
Gari lakwamisha kesi ya kina Rugemalila
Wakati huohuo, vigogo wa kampuni ya kufua umeme ya IPTL, Harbinder Sethi  na James  Rugemarila, wanaokabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi ikiwamo ya utakatishaji wa fedha, jana walikwama kufikishwa mahakamani kwa sababu ya shida ya usafiri.
Washtakiwa hao walitakiwa kufikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, wakati kesi hiyo ilipokuwa inatajwa.
Akiiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali, Emmanuel Nitume, alidai washtakiwa wote wanaokabiliwa na kesi hiyo hawakuwapo kwa sababu ya shida ya usafiri.
Ofisa wa Magereza aliyekuwamo mahakamani hapo alisisitiza kwamba washtakiwa hawakufikishwa mahakamani  kwa sababu ya shida ya magari.
Wakili Nitume alidai kesi hiyo iliyopangwa kwa ajili ya kutajwa, upelelezi wake bado unaendelea hivyo akaomba ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa.
Baada ya kusikiliza maelezo hayo, Hakimu Shaidi aliiahirisha kesi hiyo hadi  Desemba 6, mwaka huu.
Washtakiwa hao,  wanakabiliwa na mashtaka  12 ya  uhujumu uchumi  kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kighushi na  kutoa nyaraka za kughushi.
Mengine ni kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu,  kutakatisha fedha  na kuisababisha hasara ya Dola za Marekani  22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.