HASSAN DAUDI NA MITANDAO
KUNA mawili katika kila ndoa iliyodumu. Kwanza, ni uvumilivu kwa kila kinachotokea. Pili, ni ubunifu wa njia mbalimbali za kuzikabili changamoto zinazojitokeza na hata kutishia kuisambaratisha.
Wapo wanaume na wanawake wengi waliofeli katika hilo la kuzilinda ndoa zao lakini bibiye Jennifer Adams (52) na mumewe, Fraser Mackay (50), wao walisimama kidete, hatimaye wameliweza.
Si tu kuhakikisha ndoa yao inadumu, bali wamefanya hivyo kwa ‘style’ ya pekee ambayo imezua gumzo na kubaki kuwa moja kati ya habari zilizoguswa mara nyingi na vyombo vya habari vya kimataifa, likiwamo gazeti la Daily Mail la Uingereza.
Huenda ndoa ya wakazi hao wa Queensland, Australia, isingeweza kufikisha miaka 14 endapo wasingeibuka na utaratibu wao wa kutolala kitanda kimoja, chanzo kikiwa mwanamume huyo kuwa na tabia ya kukoroma.
Katika mahojiano yake na gazeti hilo kongwe, Adams anasema walifikia uamuzi huo kwa kuwa awali hakuwa akipata usingizi kutokana na tabia ya kukoroma ya Mackay, hivyo ni kama ndoa yao ilikuwa shakani.
“Unajua tulikuwa na uhusiano wa kimapenzi kwa miezi mitano tu na haraka akahamia kwangu,” anasema Adams akikumbuka kipindi ambacho walikuwa wapenzi.
Anasema iliwachukua wiki moja pekee kulala pamoja kabla ya wawili hao kukaa chini na kuja na uamuzi wa kila mmoja kuwa na kitanda chake.
“Kukoroma lilikuwa tatizo kubwa kwake. Sikuweza kulala na hata yeye alikuwa anajisikia vibaya kwa kweli, alihisi ananinyima raha,” anasema.
Mbaya zaidi, ratiba ya kazi ya Adams ilimtaka kuamka mapema, hivyo alihitaji muda mzuri wa kupumzika usiku, nafasi ambayo hakuweza kuipata kutokana na kero ya kukoroma aliyokuwa akiipata kutoka kwa ‘mshikaji’ wake, Fraser.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo na kuepusha ndoa isiyo na furaha, walianza kwa kila mmoja kulala chumba chake lakini ilipofika mwishoni mwa wiki, waliweza kutumia kitanda kimoja.
“Mwanzoni, ilikuwa noma, ilituumiza kufanya hivyo na kuna kipindi iliniliza lakini nilihitaji usingizi pia. Kipaumbele chetu kilikuwa afya, unatakiwa kuwa na afya, ndicho tulichokitaka,” anasimulia.
Kwa upande mwingine, hilo la kutokulala pamoja halikutikisa uhusiano wao kwani na kila inapofika usiku, huwa pamoja wakitwangana mabusu na hata kukumbatiana kabla ya kila mmoja kwenda chumbani kwake.
“Huwa tunahakikisha hatulali kabla ya kutakiana usiku mwema, huwa naweza hata kwenda chumbani kwake kumbusu na kumkumbatia. Huwa tunacheza kitandani na baada ya hapo kila mmoja anakwenda kulala kitandani kwake,” anasema.
Akizungumzia ndugu na marafiki wao wanavyouchukulia utaratibu wao huo, Adams anasema: “Wazazi wetu walidhani kuna ugomvi nyumbani,” anasema huku akicheka.
“Tulipowaambia marafiki na ndugu, wapo wachache walioshangaa. Lakini nafikiri huo ulikuwa ni uelewa wao juu ya kulala pamoja.”
Kwa kipindi chote cha miaka 14 cha ndoa yao, Adams anakumbuka kuwa siku pekee aliyowahi kulala kitanda kimoja na mumewe ni kipindi walichokuwa likizo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa maelezo yake kwa Daily Mail, bado alilazimika kutumia kifaa cha kusikiliza muziki masikioni kuepuka kero ya kukoroma kutoka kwa mumewe huyo.
Wakati huo huo, anasema tatizo ni kwamba wengi wamekariri kuwa ili uhusiano ufanikiwe, kuna ulazima wa mwanamke na mwanamume kulala kitanda kimoja, jambo ambalo si kweli.
Kuthibitisha hilo, anasema bado asilimia kubwa ya ndoa zinazovunjika duniani kote ni zile ambazo wahusika wake walikuwa wakilala pamoja. “Kulala vyumba tofauti hakumalizi uhusiano, ni njia ya kuboresha uhusiano,” anadai.
Adams anaamini hakuna maana ya uhusiano ambao labda mwanamke au mwanamume hawezi kupata usingizi mzuri.
“Kama unakerwa na kukoroma kwa mpenzi wako na hulali vizuri, fanya unavyoweza kujiokoa,” anasisitiza.
“Zungumza na mwenzako. Jiamini katika uamuzi wako na jivunie ulichoamua. Kama unafanya hivyo kwa sababu ya msingi, huna sababu ya kuhofia. Tambua, hufanyi hivyo kwa ajili yako, ni usingizi.”
Adams, ni mwandishi wa kitabu cha ‘Sleeping Apart Not Falling Apart’, ambacho kinahimiza wanandoa na wapenzi wanaoishi pamoja kutohofia kuacha kulala pamoja ili kuepusha kuvunjika kwa uhusiano wao.
“Ujumbe hapa ni kwamba hilo litazame zaidi afya. Kulala ni starehe na kama huipati kwa kiwango kizuri unapaswa kujiuliza. Kama mtu wako anakufa ya usilale, unatakiwa kuangalia unavyoweza kulala chumba kingine,” anaongeza.