Na Mwandishi Wetu, Songea
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa hiari na kupata chanjo ya Uviko19 hasa wazee wanandoa mwenye umri wa miaka 50 kupata Chanjo kwa sababu ni salama na imethibitishwa na watalaam wa afya.
Mwanaidi ametoa kauli hiyo wilayani Songea mkoani Ruvuma wakati wa ziara yake mkoani humo kukagua huduma za matibabu kwa wazee katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Amewataka Maofisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii kuendelea kutoa elimu na kuwahamasisha wazee kuanzia umri wa miaka 50 kujitokeza kwa hiari yao kupata chanjo ya Uviko19.
“Awamu hii ya utoaji wa chanjo ya Uviko19 tumewapa kipaumbele wazee kuanzia miaka 50 kupata chanjo ya ili kusaidia kupata kinga itakayowalinda na maambukizi ya virusi vya Corona” amesema Mwanaidi.
Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Ruvuma, Mariam Juma, amesema wataendelea kuhamasisha jamii hasa kundi la wazee na watu wenye magonjwa sugu kujitokeza kwa hiari yao kupata chanjo hiyo.
Wakati huo huo Naibu Waziri, Mwanaidi ameuagiza uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa kuwahudumia wazee wanaokuja kupatiwa huduma hospitalini hapo.