Na Malima Lubasha, Serengeti
MKUU wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Nurdin Babu amewaonya wananchi wilayani humo kuacha tabia ya kuuza chakula chote hasa mahindi kwa tamaa ya fedha na kusahau kujiwekea akiba ili kukabiliana na baa la njaa.
Babu alitoa wito huo hivi karibuni ofisi kwake wakati akizungumza na gazeti hili ambapo aliwataka wananchi kuhakikisha wanajijengea utamaduni wa kuhifadhi chakula kwani misimu ya mvua imekuwa haitabiriki na hivyo huenda mwaka unaofuata kukawa na uhaba wa chakula.
Aidha, katika hatua nyingine Babu ametoa wito kwa wananchi wote wilayani hapa kushiriki kukomesha wizi wa mazao na mifugo kwa kuimarisha ulinzi kwenye vijiji vyao na kufanya doria muda wote hasa nyakati za usuku ili kukabiliana na watu wanaojihusisha na wizi wa aina hiyo na waweze kuchukuliwa hatua.
Alisema ni lazima jamii ishiriki kuwakamata watu wa aina hiyo kisha kuwafikisha kwenye vyombo vya dola na sheria ili kudhibiti tatizo hilo ambapo aliwaonya wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga na kuwauwa.
Aidha Babu aliwahimiza wananchi kuendelea kufanya kazi na kutumia mvua zinazoendelea kunyesha sasa kulenga kupata mavuno ya chakula cha kutosha hasa mahindi ili kuepuka kujikuta kwenye baa la uhaba wa chakula.
Alisema kwa kipindi hiki ni wazi kwamba wananchi wamefanikiwa kupata mahindi ya kutosha ikiwa ni pamoja na mazao mengine lakini upo mtindo wa kuuza chakula chote na kusahau kuweka akiba kwa kipindi kijacho baadaye wakijikuta wakinunua kwa bei kubwa.
“Kila ninapopita vijijini, nikiwa katika ziara ya kukagua na kuhimiza shughuli za maendeleo wilayani maeneo ya barabara ya Nyansurura, Issenye na Ngoreme nashuhudia wafanyabiashara wengi sehemu hizo wakinunua mahindi na mtama.
“Mimi sipingi wananchi kuuza mahindi yao lakini jambo la msingi kuweka akiba na kuhifadhi vizuri matumizi ya baadaye ni muhimu ,”Alisema Babu.
Akizungumzia matukio ya uharifu, Babu aliwataka wananchi viongozi wa vijiji vyote kwa maana ya wenyeviti na watendaji kuwajibika kuzuia wizi wa aina yeyote hasa wizi wa mifugo kwa kuweka ulinzi shirikishi kuwatambua watu wanaoingia katika vijiji vyao.
Hata hivyo alitoa wito kwa wafugaji wote wa ng’ombe kuweka mazingira ya ulinzi nyumbani kwao ikiwemo kufuga mbwa watakaotoa ishara kuashiria uwepo wa matukio kama hayo nyakati za usiku na pia aliwaomba wakulima wa pamba kuuza zao hilo kwenye vyama vyao vya ushirika ( Amcos) ili inunuliwe kwa bei elekezi ya serikali.