NA SAMWEL MWANGA-MASWA
WANANCHI wameshauriwa kunywa maziwa ya ng’ombe ambayo yamepimwa na wataalamu kwa sababu ni mlo kamili.
Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dk. Fredrick Sagamiko wakati akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake.
Alisema watu wengi wamekuwa wakinywa maziwa ambayo hayajapimwa na mtaalamu wa mifugo, yanayoweza kusababisha magonjwa mbalimbali kwa binadamu, ikiwamo kifua kikuu.
Dk. Sagamiko alisema wananchi wengi wamekuwa wakikumbwa na maradhi mbalimbali kutokana na unywaji holela wa maziwa yasiyo na kiwango.
Kutokana na hali hiyo, alisema halmashauri hiyo imeona ipo haja ya kuanzisha vituo vya kukusanyia maziwa ambavyo vitafanya kazi ya kuyapima kutoka kwa muuzaji kabla ya kwenda kwa mnunuzi.
“Tumeona ipo haja ya kuanzisha vituo vya kukusanyia maziwa ili maziwa yanapotoka kwa muuzaji ambaye ni mfugaji au mfanyabiashara yapitie kwanza kwenye kituo yapimwe ili kujua ubora wake kabla ya kununuliwa na mtumiaji, tunafanya hivi ili kulinda afya zetu,” alisema Dk. Sagamiko.
Alisema kumekuwepo na wananchi ambao ni wafugaji wasiokuwa waaminifu, wakijua ng’ombe wamewapatiwa dawa kwa ajili ya magonjwa mbalimbali, wanawakamua maziwa na kwenda kuuza kwa lengo la kupata fedha.
Aliwashauri wajumbe wa kamati ya lishe ya wilaya kabla ya kuanzishwa kwa kituo hivi karibuni, kuhamasisha wananchi kutumia maziwa ambayo yamechemshwa kabla ya kuyatumia.
Ofisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Efreim Lema alisema tayari maeneo mengine nchini, wameanzisha vituo hivyo na kuwasaidia wananchi kunywa maziwa bora.
Alisema watajitahidi kuendelea kuwahamasisha wananchi kuhusu unywaji wa maziwa ambayo ni salama kwa afya zao kwa sababu wamegundua wengi wao wamekuwa wakinywa bila kuchemshwa hali ambayo ni hatari kwa afya zao.
“Wananchi wengi wilayani wamekuwa wakitumia maziwa bila kuchemshwa, hali si salama kwa afya zao, tutaendelea kuwahamasisha kabla ya kunywa, ninyi wajumbe wa kamati hii tusaidiane kuhamasisha jambo hili,” alisema Lema.