31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Changamoto ya mimba shule za msingi, sekondari Shinyanga kubwa

Na Ali Lityawi – Kahama

IMEELEZWA bado kuna changamoto kubwa ya mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari mkoani Shinyanga.

Hii inatokana na jamii kutokuwa tayari kufundisha vijana wao afya ya uzazi kwa imani kuwa wanakiuka mila na desturi.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mratibu wa Uzazi wa Mama na Mtoto Mkoa wa Shinyanga, Joyce Kondoro wakati wa kuhitimisha mafunzo ya afya ya uzazi kwa vijana na ukatili wa kijinsia kwa vijana 72 kutoka shule 18 za halmashauri tatu za mkoani hapa.

Joyce alisema uwapo wa uvumi potofu pindi vijana wanapofundishwa elimu ya afya ya uzazi, wanapelekwa njia isiyostahili kwa mila na desturi, hivyo kuomba kuondokana na dhana hiyo ili kufikisha elimu itakayokuwa msaada mkubwa kwa vijana kufikia ndoto zao za maisha.

Aliliomba Shirika la World Vision na asasi zingine za kiraia ziongeze kasi kushirikiana na Serikali kukabiliana na mimba za utotoni ambazo zimekuwa sababu ya kurudisha nyuma maendeleo ya taifa.

Alisema vijana ni vema wakatambua umuhimu wa afya ya uzazi wakiwa katika rika lao kutokana na wengi wao kutofahamu suala hilo kwa kina.

Joyce alisema mafunzo ya afya ya uzazi kwa vijana, yataepusha mimba na ndoa  za utotoni.

Alisisitiza elimu hiyo itasaidia vijana kuondokana na mila potofu iliyojengeka kuwa ni sehemu ya maisha, huku ikiwa sababu ya kukatisha masomo yao na kukatili ndoto za maisha yao.

“Tunaona kuna wanafunzi wengi vijana wanaopata ukatili, wanaofanyiwa ukatili na kutojua ni ukatili, wanaona ni sehemu ya maisha lakini kwa kupata elimu watatambua huo ni ukatili na wafanye nini ili kukabiliana nao,” alisema Joyce.

Alisema ni muhimu kuwepo  mawasiliano mazuri baina ya walimu na walezi ili kubaini changamoto zinazowakabili wanafunzi na kuwapatia ushauri utakaowawezesha kukabiliana na matatizo hayo.

Joyce alisema mabadiliko ya makuzi kwa vijana yasiposimamiwa na vijana wenyewe kwa msaada wa wazazi na walimu, inakuwa changamoto kubwa ya kukatisha ndoto zao kwa kushindwa kudhibiti mihemko ya ujana ambayo athari yake uonekana uzeeni.

Ofisa Jinsia na Utetezi wa Mradi wa Enrich, unaotekelezwa na World Vision Tanzania kwa msaada wa Serikali ya Canada, Magreth Mambali alisema wametoa mafunzo kwa walimu wa afya na malezi 18 ili wasaidie wanafunzi hao kufikisha elimu sahihi itakayosaidia kuibadili jamii.

Mratibu wa Mradi  kutoka World Vision, Dk. Frank Mtimbwa alikiri kuwepo kwa tatizo kubwa la ukatili wa kijinsia Shinyanga, huku wakitoa mafunzo katika eneo dogo la shule tisa za msingi na tisa za sekondari katika halmashauri za wilaya za mkoa huo na Kishapu na mji wa Kahama, kulingana na ukubwa wa mradi.

Alisema mkakati wa shirika lake, mradi ujao ni kufika kila kijiji na shule kwa halmashauri za mkoa mzima, hatua itakayosaidia kuondokana na tatizo la ukatili wa kijinsia na mimba za utotoni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles