28 C
Dar es Salaam
Friday, February 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi Ngara kupatiwa vitambulisho vya Taifa

Na Allan Vicent, Ngara

Mbunge wa Jimbo la Ngara mkoani Kagera, Ndaisaba Ruhoro, ameanza kutekeleza ahadi alizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, Mwaka jana kwa kumaliza tatizo la upatikanaji wa vitambulisho vya uraia.

Akizungumza na www.mtanzania.co.tz amesema kuwa suala la vitambulisho vya uraia kwa wakazi wa jimbo hilo ni muhimu sana kwani wengi wao wamekuwa wakikamatwa mara kwa mara na Maofisa wa Uhamiaji wakidhaniwa kuwa ni wahamiaji haramu.

Alisema kuwa aliahidi kumaliza tatizo hilo punde tu atakapochaguliwa kuwa mbunge wao hasa kutokana na jimbo hilo lililoko mpakani mwa nchi za Rwanda na Burudi kuwa na mwingiliano mkubwa wa raia wa kigeni kutoka mataifa hayo.

Amebainisha kuwa kutokuwepo kwa mipaka inayoonekana ili kutenganisha wilaya hiyo na nchi jirani imekuwa changamoto kubwa ambayo hupelekea raia wa kigeni kuingia nchini kupitia sehemu yoyote ile pasipo kutambulika.

Ruhoro amesisitiza kuwa suala la mipaka katika eneo hilo bado ni tatizo lakini akabainisha kuwa ili kutambua wakazi halali kila mkazi wa jimbo hilo ameandikishwa na Maofisa wa NIDA ili kupewa kitambulisho cha uraia.

“Inaumiza sana unapoambiwa kuwa wewe siyo Mtanzania wakati umezaliwa hapa hapa Tanzania na wazazi wako wote ni Watanzania, kwa sababu tu ya raia wanaoingia bila kibali cha uhamiaji kutoka nchi jirani,” amesema Ruhoro.

Aidha, amesisitiza kuwa Wilaya hiyo ni kubwa na ina wananchi wengi, hivyo huwezi kutambua raia na asiye raia kwa kuwaangalia tu, ila vitambulisho vya uraia vitasaidia sana kuondoa sintofahamu hiyo, kwa sasa vinaandaliwa ili wapewe.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo ambaye ni Mkuu wa wilaya hiyo, Lt Kanali Michael Mntenjele, alisema mwingiliano wa raia wa kigeni wilayani humo unahatarisha maisha ya wananchi na nchi kwa ujumla.

Alibainisha kuwa wamekuwa wakijitahidi sana kuimarisha ulinzi katika mipaka ya wilaya hiyo na nchi jirani, ila changamoto iliyopo ni wahamiaji kuingia nchini kupitia njia za panya, japokuwa wanapokamatwa sheria huchukua mkondo wake.

“Tunampongeza sana mbunge wetu kwa hatua anazochokuwa katika kuhakikisha kila raia halali anapata kitambulisho, hii itasaidia kuwabaini wahamiaji haramu na kuwachukulia hatua zaidi za kisheria,” amesema Mntenjele.

Wakazi wa wilaya hiyo wamepokea kwa furaha kubwa hatua ya Maofisa wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kupita katika vijiji na kata zote kuandikisha wakazi wote wa jimbo hilo ili kupatiwa vitambulisho hivyo.

James Minani, mkazi wa kata ya Kabanga aliomba vitambulisho hivyo kuharakishwa ili kuwaondolea usumbufu kutokana na kamata kamata ya wahamiaji haramu ambapo hata wakazi halali hujikuta wakikamatwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles