NA Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Wananchi wilayani Kigamboni mkoani Dar es Salaam wametakiwa kuzungumza na watoto kuhusu mambo mbalimbali ya kijamii ili kuwalinda na kuwaepusha na vitendo vinavyosababisha mmomonyoko wa maadili.
Wito huo umetolewa June 19 na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo wakati wa ziara yake ya mtaa kwa mtaa inayoitekeleza wakati wa ziara yake ya kuzungumza na wananchi ili kujua na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili ambazo ameanza kwenye mtaa wa mkamba uliopo kata ya Kisarawe II.
Amesema Serikali ya awamu ya sita imeweka mazingira bora kuanzia ngazi ya jamii hivyo viongozi katika mitaa na kata wanapaswa kuwasikiliza wananchi na kuwasaidia kwenye changamoto zao.
“Ofisi yake inapokea kesi mbalimbali za mmomonyoko wa maadili zinazowahusu watoto zaidi ya 2,000 pamoja na watu wazima zaidi ya 120, hivyo walezi na wazazi wanapaswa kuongea na watoto wao kuhusu maadili Kwani mabadiliko yanaanza na wao katika ngazi ya familia,” amesema Halima.
Aidha, amewataka wakazi wa mtaa huo kutojihusisha na suala la uhalifu na wafugaji kutolisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima ili kuepukana na migogoro inayojitikeza baina ya wakulima na wafugaji.
Nae Afisa Mifugo na Uvuvi Manispaa ya Kigamboni, Aaron Bullu amesema kuna Sheria mbalimbali za ufugaji ikiwemo mfugaji anatakiwa kua na eneo la ufugaji zaidi ya Square Mita nne.
Baadhi ya Wananchi wameiomba serikali kuwaleta kwa karibu huduma muhimu kama shule, zahanati na kutatua kero ya umeme wanayoipata.