Na Nyemo Malecela, Kagera
Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata amewataka wananchi wa Mkoa wa Kagera kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuwa walinzi wa mipaka inayouzunguka mkoa huo ili kudhibiti biashara za magendo.
Kidata ameyasema hayo kwenye kikao chake na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, watumishi wa TRA, viongozi wengine wa serikali na wafanyabiashara mkoani humo kilicholenga kufahamu changamoto zinazowakabili walipa kodi na kujadiliana jinsi ya kuzitatua.
Kidata alisema mikoa iliyoko pembezoni inakabiliwa na changamoto ya bidhaa kutoka nchi jirani kuingizwa nchini bila kulipiwa ushuru.
“Ni vizuri kila mwananchi akawa balozi kwa kuhakikisha bidhaa ambazo hazipitishwi kwenye forodha kwa ajili ya kulipiwa ushuru hazitumiki kwani mbali na dhana ya kupoteza mapato lakini pia bidhaa hizo sio salama kwa afya ya wananchi kwani hazipimwi kama zinafaa kwa matumizi ya binadamu,” alisema Kidata.
Pia Kidata aliwashauri wafanyabiashara kuwa ili waepukane na changamoto ya kusumbuliwa na TRA ni lazima wazingatie utunzaji wa kumbukumbu sahihi na kutumia mashine ya EFD ili watakapofanyiwa makadirio yawe na uhalisia wa kipato chao.
Na kuhusu mashine za EFD ambazo wafanyabiashara walidai zimekuwa changamoto zinapoharibika, aliwasisitiza wafanyabiashara wanatakiwa kutoa taarifa TRA zinapoharibika ili hatua stahiki zichukuliwe ikiwemo mawakala waweze kuzitengeneza kwa haraka au kuwabadirishia ili ziweze kuendelea kutoa huduma.
Aliongeza kuwa kwa sasa TRA iko kwenye mchakato wa kuhakikisha wafanyabiashara wanatumia vifaa vingine vya ziada tofauti na mashine za EFD.
“Kuna mfumo umeshatengenezwa na uko kwenye majaribio ambao utamwezesha mfanyabiashara kutumia vyombo vingine vya uhasibu ikiwemo simu za mkononi kuweza kutoa risiti za kielekroniki na kufikia mwaka wa fedha ujao tunatarajia utakuwa umeanza kutumika rasmi,” amesema.
“Na kuhusu suala la magendo bado tunalishughulikia kwenye mipaka yote ili kuhakikisha mlaji anapata bidhaa salama lakini pia kuweza kulinda mapato yetu kupitia kodi ili kuboresha maendeleo ya Mkoa.”
Mbuge aliwataka wafanyabiashara wa Mkoa wa Kagera kutoa ushirikiano ofisini kwakwe endapo watakuwa na taarifa za wafanyabiashara wakubwa wanaowatumia wafanyabiashara wadogo kuingiza bidhaa nchini kwa njia za magendo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania kwa Mkoa wa Kagera, Jovinus Basimaki alisema licha ya mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kukusanya mapato mengi lakini umekuwa wa mwisho katika maendeleo ukilinganisha na kodi inayokusanywa.
“Ukilinganisha takwimu za watu na makusanyo ya kodi havifanani kabisa na maendeleo ya kiuchumi yaliyopo mkoani Kagera, tumekuwa miongoni mwa mikoa inayokusanya kodi nyingi lakini pia tumekuwa wa mwisho kimkoa katika suala la maendeleo,” alisema.
Pia aliishauri TRA kuwa ili kukomesha magendo inabidi serikali ya Tanzania kwa kushikiana na nchi jirani kuweka soko la pamoja kwa ajili ya biashara ambazo hazipatikani nchini jambo litakalosaidia wafanyabiashara wote kwenda katika soko hilo kwa ajili ya kupata bidhaa hizo hivyo TRA itaweza kukusanya kodi kwa urahisi kupitia soko hilo.
Wakati naye Pili Makunenge ambaye ni mfanyabiashara kutoka wilayani Biharamulo alisema elimu inayotolewa na TRA kwa walipa kodi bado haitoshelezi na imekuwa ya zima moto.
“Mfano inatolewa taarifa saa tano asubuhi kwamba kutakuwa na elimu kwa mlipa kodi saa nane mchana, kitu ambacho hakistahili kwani muda huo mfanyabiashara anakuwa anaandaa ratiba yake ya kesho hivyo wengi wao hawatahudhuria.
“Pia kumekuwepo na changamoto ya bidhaa zinazotoka nchi jirani ambazo zinafanana na bidhaa zinazozalishwa hapa nchini. Mfano ni sabuni zilizopo mtaani nyingi zinatoka nchini Uganda na Burundi ambazo zinauzwa kwa bei nafuu kuliko zinazozalishwa hapa nchini.
“Hii inaonyesha kuna udhaifu kwa watumishi wa TRA katika kutoza kodi katika bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi jambo linalosababisha wazalishaji wa ndani kuwa na kiwango kidogo cha mauzo kutokana na bidhaa zao kuuzwa kwa bei kubwa kutokana na kulipia kodi,” alieleza Pili.
Pili aliongeza kuwa kwa wafanyabiashara wanaopeleka bidhaa zinazozalishwa nchini kwenda kuuzwa nchi jirani wamekuwa hawatozwi VAT, lakini wamekuwa sio waaminifu kwani wamekuwa hawafikishi bidhaa hizo katika nchi zinazotakiwa kwenda na badala yake zinarudishwa nchini na kuuzwa kwa bei nafuu hali inayopelekea wafanyabiashara waliolipa VAT kushindwa kuhimili ushindani wa soko kwa bidhaa hizo.