27 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kiwango cha matatizo ya kuona yanayoepukika kimepungua-Dk. Gwajima

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk.Dorothy Gwajima, amesema kuwa kiwango cha matatizo ya kuona yanayoepukika kwa ujumla kimepungua duniani huku Tanzania inakadiriwa kuwa na watu 640,000 wasioona.

Waziri Gwajima amebainisha hayo jana Jijini Dodoma wakati wa kilele cha siku ya afya ya macho Duniani ambapo amebainisha kuwa watu zaidi ya milioni 2.4 wenye matatizo ya kutokuona huku asilimia 55 ya matatizo haya yanawaathiri wanawake.

Dk.Gwajima amesema visababishi vikubwa vya ulemavu wa kutokuona na upungufu wa kuona unaoweza kuzuilika kama vile upeo mdogo wa macho kuona na uoni hafifu vinavyorekebishika kwa miwani, mtoto wa jicho na shinikizo la jicho.

“Taarifa ya Shirika la Afya Duniani imeonyesha kuwa idadi kubwa ya watu wenye matatizo ya kutokuona asilimia 89 wanaishi katika nchi za uchumi wa kati na wa chini, Tanzania ikiwa miongoni mwa hizo”, ameeleza Waziri Gwajima.

Aidha, watu wenye matatizo ya kutokuona kwa viwango vya kati na juu wanakadiriwa kuwa ni mara tatu ya watu wasioona ambao ni takriban watu milioni 1.8.
“Kwa ujumla Tanzania ina watu zaidi ya milioni 2.4 wenye matatizo ya kutokuona. Asilimia 55 ya matatizo haya yanawaathiri wanawake.

Visababishi vikubwa vya ulemavu wa kutokuona na upungufu wa kuona unaoweza kuzuilika kama vile Upeo mdogo wa Macho kuona na uoni hafifu vinavyorekebishika kwa miwani, mtoto wa jicho na Shinikizo la jicho,” amesema Dk.Gwajima.

Dk.Gwajima ameongeza kuwa takwimu za hapa Tanzania zinaonyesha watu milioni 1.2 tu kwa mwaka 2020 ndio walifikiwa na huduma za macho katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya ikilinganishwa na uhitaji wa takribani watu milioni 12,000,000.

“Na kati yao, asilimia 32% wanakuwa tayari wana upungufu wa kuona ikijumuisha ulemavu wa kutokuona. Upasuaji wa mtoto wa jicho kwa mwaka jana ulifanyika kwa wastani wa macho 200 tu kwa kila watu milioni 1, ikilinganishwa na macho 2,000 kwa kila watu milioni 1 kama inavyoshauriwa na Shirika la Afya Duniani,” amebainisha. Waziri Gwajima.

Ameongeza kuwa asilimia 38 tu ya watu wenye uhitaji wa miwani ya kurekebisha uoni ndiyo waliweza kupata miwani hiyo kutoka kwenye vituo vya tiba.

Aidha,Dk. Gwajima amesema kwa mwaka huu, Wizara ilipanga kuelimisha jamii na viongozi pia kuhimiza watu kupima macho kupitia vituo mbalimbali.

Maadhimisho ya siku ya kuona duniani ya mwaka huu yamekuwa tofauti sana kwa sababu ni mwaka mwingine tangu kuisha kwa utekelezaji wa Mkakati wa Kimataifa wa Dira ya mwaka 2020. Mkakati mpya umeandaliwa uliojikita kwenye Mapendekezo Taarifa ya Dunia ya Uoni iliyoandaliwa na ya Shirika la Afya Duniani.

Dk. Gwajima amewaasa wananchi kujizuia kupata matatizo ya macho, kuepuka kuweka kwenye macho dawa ambazo hujaandikiwa na wataalamu kutoka kwenye Hospitali na vituo vya tiba au dawa zisizo rasmi.

Hata hivyo amesema kuwa kuhifadhi hali ya uoni ikiwa ni pamoja na kupanga angalao siku moja kwa mwaka kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kina wa afya ya macho yako yaani kupimwa uwezo wa kuona, upeo wa macho kuona na pia kipimo cha ndani ya jicho.

“Ifanye Afya ya Macho kuwa kipaumbele, hakikisha kuwa swala la upimani wa macho ni sehemu ya huduma ya Afya inayotolewa kwenye eneo lako. Penda Macho yako ni Utume wa Maisha,”amesisitiza Waziri Gwajima

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Christian Blind Mission Tanzania (CBM) Bi Nesia Mahenge amesema tatizo la uoni hafifu na upofu linapelekea jamii kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na maendeleo ya jamii na kuzidi kuongeza tatizo la umaskini Tanzania.

Pia, amesema Tanzania kuna changamoto ya upungufu wa rasilimali watu wa kutoa huduma ya afya ya machoa ambapo amedai Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 75 ya matatizo ya uoni hafifu na upofu Tanzania yanazuilika.

“Tunaiomba Serikali kwenye sera ya Afya na miongozo ya kuandaa bajeti na mahitaji ya Afya ya Macho iainishe vema kipengele cha Afya ya Macho na kukipa uzito unaostahili. Wadau tunaiomba Serikali ihakikishe kuna uwepo wa rasilimali watu kwenye ngazi zote za Taifa ili kurahisisha wadau kufika maeneo,” amesema Mahenge.

Akisoma taarifa ya hali ya uoni duniani,Mkurugenzi wa Shirika la Sightsavers,Godwin Kabalika amesema uoni unabaki kuwa mlango mkubwa wa fahamu katika kila hatua ya maisha ya mwanadamu.

“Mtoto anayezaliwa anategemea uoni kutambua na kuweka mahusiano karibu na mama mtoto anayeanza kutembea pia anahitaji uoni ili aweze kujifunza na hatua zake hali kadhalika mtoto wa shule anapoenda shule na vijana wanahitaji uoni ili kujitegemea hata watu wazima wanahitaji uoni,” amesema Kabalika.

Amesema matatizo ya macho bado yapo na kwa kiasi kikubwa kila mmoja hupata tatizo la macho amedai kwa miaka ijayo idadi ya tatizo litaendelea kukua kutokana na uongezeko la watu mabadiliko ya tabia Nchi.

Amesema Mifumo ya afya inakabiliwa na changamoto ya kufikia uhitaji wa sasa na unaotarajiwa duniani na ili kukabiliana na ongezeko hilo kunahitajika kuongezeka kasi za afua kukabiliana na changamoto hizo.

“Mapendekezo ya taarifa hiyo ni pamoja na afya macho iwe sehemu afya kwa wote,kujumuisha afya ya macho kwenye huduma za afya kwa kumlenga mhitaji ,kuhamasisha tafiti ya utekelezaji wa viwango vya juu na kuongeza uelewa,kufanya ufuatiliaji na tathimini ya maendeleo,kuongeza uelewa na kushirikishwa watu na jamii,” Kabalika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles