28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi wenye ualbino wajipanga kukabili changamoto za wenzao

 CLARA MATIMO – MWANZA 

BAADHI ya wanafunzi wenye ualbino wanaofadhiliwa masomo na Taasisi ya The Foundation of Josephat Torner Europe Aid (Fojotea), inayotetea haki za watu walioko pembezoni, wamedhamiria kupunguza changamoto zinazowakabili wenzao katika maisha yao ya kila siku. 

Walibainisha hayo jijini hapa jana walipozungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti kuhusu mustakabali wao baada ya kuhitimu masomo na waliishukuru Fojotea kwa kuwafadhili maana wanaamini watatimiza ndoto na malengo yao.

Walisema masomo wanayosoma yamejikita katika falsafa ya uongozi wa jamii, hivyo itakuwa ni muda mwafaka kwa wao kushirikiana na Serikali pamoja na taasisi zingine binafsi kutokomeza unyanyapaa ambao umekithiri miongoni mwao. 

Enock Kusekwa, mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya Longido mkoani Arusha, alisema anatarajia kusomea sheria ili aweze kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu wakiwamo wenye ualbino ambao wanaporwa haki zao za msingi. 

 “Watoto wengi wenye ulemavu wakiwemo albino wamekosa haki ya kuishi na kupata matunzo kutoka kwa wazazi wao, hasa baba kwa sababu tu wamezaliwa na hali hizo, hivyo wamewakataa wao pamoja na mama zao. Hata mimi ni muhanga wa hilo.

“Mimi nimepitia manyanyaso mengi sana kutoka kwa wanajamii na baadhi ya ndugu zangu, tukio ambalo sitalisahau maishani ni siku niliyopewa chakula na bibi yangu wa kambo kilichokuwa kimepikwa kwa ajili ya mbwa, nikaambiwa nile kwa sababu sina tofauti na mnyama huyo,” alisema Kusekwa. 

Pius Boniphace na Yohana Bahame, walisema ndoto zao ni kuwasaidia wengine wenye ulemavu hata kwa mawazo ili waweze kutimiza malengo yao, lakini wakipata nafasi ya kufanya kazi katika ngazi za maamuzi watafurahi zaidi kwa sababu watashiriki kikamilifu kulinda haki na masilahi ya kundi hilo. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Fojotea, Josephat Torner, alisema hadi sasa wamekwisha wafadhili masomo wanafunzi 14 kuanzia ngazi ya msingi, sekondari na vyuo vikuu kwa sababu wanaamini ukimwezesha mtoto kupata elimu bora, unatengeneza kizazi chenye weledi na uadilifu. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles