NA ELIYA MBONEA
-KIA
WANAFUNZI watatu majeruhi wa ajali ya basi la Shule ya Msingi Lucky Vincent iliyoua watu 35, wamesafirishwa kwenda Marekani kwa matibabu zaidi chini ya ufadhili wa Shirika la Samaritan’s Purse.
Majeruhi hao watapatiwa matibabu Hospitali ya Mercy iliyopo Jiji la Sioux, IOWA ambapo watafanyiwa matibabu ya kina ya mifupa kutokana na majeraha waliyopata ikiwamo kuvunjika mifupa ya miguu, mkono, taya, shingo na nyonga.
Msafara wa majeruhi hao ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo uliondoka jana katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru Saa 1 asubuhi kwa mabasi matatu tofauti ya kubeba wagonjwa.
Kutokana na aina ya majeruhi hao, msafara huo uliokuwa na magari zaidi ya 10 yakiwamo ya familia, viongozi wa mkoa, madaktari na ndugu wanaosafiri uliwasili KIA Saa 2:45 asubuhi.
Wakiwa uwanjani hapo huku kwaya ya nyimbo za injili ikiendelea kutumbuiza na kuwatia faraja wazazi na ndugu wa marejeruhi ambapo kazi ya kuanza kuwaingiza ndani ya ndege majeruhi hao ilianza saa 4:20 asubuhi.
Gari maalumu (winch), iliyokuwa uwanjani hapo ilianza kuwabeba majeruhi hao tayari kwa kuwaingiza ndani ya ndege ikianza na Wilson Tarimo, akifuatiwa na Sadia Aawadhi na kisha Doreen Mshana.
Hadi kufikia Saa 5:15 shughuli ya kuwaingiza majeruhi hao ilikuwa imekamilika na huku tayari wazazi wote, daktari na muuguzi wanaosafiri wakiwa tayari wameingia ndani ya ndege aina ya DC 8 N 782 SP.
Kukamilika kwa shughuli hizo ikiwamo Mratibu wa safari Lazaro Nyalandu kusaini kibali cha kuruka ndege iliyoongozwa na Captain Brian Hilliard, ikimilikiwa na Sammaritan’s Purse, International Relief, (Helping in Jesus Name) kulitoa fursa ya kuanza safari Saa 5:50 ya kuelekea Marekani.
WAZAZI
Wakizungumza kwa machungu uwanjani hapo huku mama wa watoto hao wakiendelea kugubikwa na majonzi, ambapo Baba wa watoto hao walishukuru juhudi zilizofanywa kufanikisha safari hiyo.
Akizungumza uwanjani hapo baba wa Sadia, Awadhi Mohame alisema, anashukuru kwa msaada mkubwa uliotolewa na serikali, wadau mbalimbali na Mfuko wa Samaria kwa kuhakikisha maisha ya watoto wao yanaimarika.
“Natarajia watoto watarudi salama tuzidi kuwaombea,”alisema Mohamed.
Kwa upande wake Baba wa Doreen, Elibariki Mshana alisema wana kila sababu ya kumchukuru Mungu kwa kile kilichotokea.
“Tusihukumu katika jambo lolote bali tushukuru kwa kila jambo lililotokea,” alisema Mshana.
Naye Baba wa Wilson, Godfrey Tarimo alisema mtoto wake anaendelea vizuri hivyo ana imani atapona.
Afya za majeruhi hao ziliendelea kuimarika tangu walipokuwa wodini kwani walianza kuzungumza huku wakibadilishana mawazo wao kwao, bila kujua kama wanafunzi wenzao walipoteza maisha kwenye ajali hiyo.
Awali akizungumza uwanjani hapo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, aliwashukuru wadau wote waliojitokeza kushirikiana na Serikali katika jambo hili gumu la kuokoa roho za watoto hao.
“Kazi hii tumeifikisha nusu hasa baada ya kukamilisha ile ya kuaga miili ya wanafunzi na walimu pale uwanjani, ndugu zangu jambo hili si la kisiasa kabisa.
“Kuna wanaotumia mitandao ya kijamii kupotosha lengo, nia yao ni kuturudisha nyumba ili tushindwe kusaidia watoto na juhudi za serikali za kuokoa maisha ya wanafunzi hawa.
“Tusikubali mtu atutoe kwenye jambo la msingi. Nakushuru mheshimiwa Nyalandu na Wamarekani waliojitoa kwa jambo hili.
“Pia Serikali kupitia kwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu upatikanaji haraka wa hati za kusafiria,” alisema Gambo.
Mratibu wa safari hiyo Lazaro Nyalandu ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Taasisi ya Stemm iliyowaleta nchini madaktari waliotoa msaada wa kwanza eneo la ajali wilayani Karatu alisema, kazi iliyobakia kwa sasa ni ndogo.
“Namshukuru Mkurugenzi wa Mfuko wa Msamaria Frankline Graham kutoa ndege iliyochukua watoto majeruhi.
“Fedha zinazochangwa na shule tatu za Arusha, Shule ya Kimataifa ya Moshi (ISM), St. Costantine na Braeban zitapelekwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kujenga chumba cha kupokelea wagonjwa mahututi(ICU),” alisema Nyalandu.
Akifafanua kuhusu safari hiyo Nyalandu alisema mara baada ya kuondoka KIA itakwenda moja kwa moja hadi uwanja wa ndege wa Charllotte iliopo Jimbo la North Calorina nchini Marekani ikiwa ni safari ya zaidi ya Saa 20.
Wakiwasili uwanjani hapo Mfuko wa Msamaria umeandaa ndege nyingine maalumu (Air Ambulance) itakayoondoka uwanjani hapo kuelekea Hospitali ya Mercy iliyopo Jiji la Sioux Jimbo la IOWA,” alisema Nyalandu.