21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

WANAFUNZI LUCKY VINCENT WAAMSHA MACHOZI YA FURAHA

ELIYA MBONEA NA JANETH MUSHI

-KIA

VILIO vilivyoambatana na vicheko jana vilitawala Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), wakati makundi mbalimbali ya watu, wakiwamo wananchi, wazazi na ndugu, walipojitokeza kuwalaki watoto watatu manusuru wa ajali ya basi la Shule ya Lucky Vincent, iliyotokea Mei 6, mwaka huu na kuua wanafunzi 32, dereva mmoja na walimu wawili.

 

Watoto hao, Doreen Mshana, Wilson Tarimo na Sadia Awadhi, ambao walikuwa wakipatiwa matibabu nchini Marekani kwa takribani miezi mitatu, waliwasili kwa Ndege DC 8 N782SP ya Shirika la Samaritan’s Purse.

Ikiwa pia imewabeba madaktari na wazazi wa watoto hao, ndege hiyo iliwasili KIA saa 3:33.

Kutokana na kila aliyekuwa uwanjani kutaka kuwaona watoto hao, ambao waliondoka wakiwa vitandani, lakini sasa wanatembea, askari polisi na maofisa wa uwanja huo walijikuta katika wakati mgumu wa kuzuia watu waliokuwa wanasukumana.

 

SHANGWE

Aliyeanza kushuka na kuamsha hisia za shangwe ni kijana Wilson Tarimo, aliyekuwa ameongozana na Sara, ambaye ni mtoto wa waziri wa zamani na Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu, aliyekwenda kumpokea ndani ya ndege hiyo.

Wilson akiwa mwenye furaha zaidi, aliwapungia wananchi, kisha kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, aliyemwakilisha Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu.

Wilson, aliyekuwa akitabasamu muda wote, alisema maneno machache tu, “Naishukuru Serikali ya Tanzania na Marekani, Mungu awabariki sana, asanteni sana.”

Wa pili kushuka ambaye aliamsha furaha iliyozidi na hivyo wengi kujikuta wakitokwa na machozi ni Sadia, ambaye naye aliwapungia wananchi.

Sadia akiwashukuru watu waliojitokeza uwanjani hapo, alisema: “Ninawashukuru sana kwa kuja na kuendelea kuniombea, Mungu awabariki wote”.

 

Manusura wa tatu kushuka ndani ya Ndege alikuwa ni Doreen, ambaye alionekana kugusa zaidi mioyo wa wananchi waliojitokeza uwanjani hapo, kutokana na kuwa ndiye majeruhi aliyekuwa ameumia zaidi sehemu za mwili wake.

Doreen alishuka akitembea mwenyewe, na wakati mwingine akisaidiwa kidogo kushikiliwa na daktari wake.

Mtoto huyo aliondoka nchini akiwa majeruhi zaidi kutokana na kuvunjika nyonga, taya na uti wa mgongo, ambapo baada ya kushuka alilazimika kutumia baiskeli maalumu.

Akizungumza uwanjani hapo, Doreen alisema maneno matatu; “Asante, Mungu awabariki na Mungu awabariki wote kwa kujitoa kwenu.”

 

ENEO LA UWANJA

Shughuli ya kuwapokea manusura wa ajali hiyo, iliyoacha simanzi kwa Taifa, ilifanyika eneo la Magharibi mwa Uwanja huo, kwa kuhusisha kwaya, wakiwamo waimbaji maarufu, Angel Bernald na Mercy Masika kutoka Kenya, huku mshereheshaji akiwa Msanii wa vichekesho, Massanja Mkandamizaji.

 

Miongoni mwa wageni mbalimbali waliofika uwanjani hapo ni pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro, Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wa dini mbalimbali.

 

RC KILIMANJARO

 

Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais, Mghwira alijikuta akitokwa na machozi wakati akisoma hotuba yake mbele ya watoto hao.

Pengine kwa kuguswa na mazingira ya tukio na matibabu ya watoto hao, alisema: “Ninasema kwa kulia kwa uchungu, kama mama na kama mzazi ninatambua, ninaomba watoto hawa wawe ushuhuda wa maisha mema. Wakawe ushuhuda kwa madaktari wetu na wauguzi wanaoiba dawa na vifaa hospitalini.

 

“Wauguzi hawa wanalazimisha wagonjwa kununua huduma, inatia uchungu inauma. Naomba watoto hawa wakawe utu na uzalendo wa Taifa letu,” alisema Mghwira.

 

Alisema kwa kuwa Shirika la Stemm lililowahudumia watoto hao limeanzisha mfuko maalumu wa The Tanzania Miracle Children Fund ili kuwasomesha hadi vyuo vikuu, hivyo Serikali katika kuunga mkono hilo imemwelekeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, kuzitoa Sh milioni 20  zilizokuwa zimebaki kwenye rambirambi kwa ajili ya kutunisha mfuko huo.

Mghwira pia aliushukuru uongozi wa Stemm, ambao walitumia ndege iliyowabeba watoto hao kuleta pia vifaa mbalimbali vya tiba vitakavyopelekwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.

“Tusishukuru kwa maneno, bali kwa vitendo kuanza kuwajibika, kwani sisi pia tungeweza kuwahudumia watoto na gharama zake zingekuwa tofauti.

 

“Lakini kwasababu ya ubadhirifu wetu na tabia zetu za kibinafsi, tumeshindwa kutunza rasilimali kwa kiwango hiki cha kuokoa maisha ya watoto watatu tu. Achilia maisha ya wengi yanayopotea kwa ajali,” alisema.

 

NYALANDU

Kwa upande wake, Mratibu wa shughuli hiyo na Mwenyekiti mwenza wa Shirika la Stemm, Nyalandu, akizungumza uwanjani hapo, alisema shirika hilo limetoa msaada wa vifaa mbalimbali vya hospitalini pamoja na dawa, lengo likiwa ni kusaidia juhudi za serikali.

“Na leo tumeleta vifaa mbalimbali na dawa zaidi ya tani 37,000,” alisema.

 

Akizungumzia gharama iliyotumika kwa ajili ya matibabu ya watoto hao, alisema hakuna fedha taslimu iliyotolewa kuwahudumia, kwani kila hatua iliyokuwa ikihitajika malipo yake tayari wahusika walishajitolea.

 

“Matibabu na gharama nyingine, zikiwamo za usafiri, ni zaidi ya Dola za Marekani 800,000, ambayo ni sawa na Sh bilioni 1.7,” alisema Nyalandu.

Nyalandu ndiye aliyekuwa mratibu wa safari za matibabu kwenda nchini Marekani kupitia Shirika la Stemm, ambapo kupitia ushiriki huo, alitumia pia Shirika la Samaritan Purse kuomba msaada wa ndege kwa ajili ya kuwasafirisha majeruhi hao.

Akizungumzia ushiriki wa serikali katika safari ya matibabu ya watoto hao, alisema;

“Ilikuwa si rahisi kwa Ubalozi wa Marekani kutoa VISA siku ya Jumapili, lakini Serikali ilihusika na kuhakikisha VISA zinapatikana, lakini pia ilitoa daktari bingwa wa mifupa, Dk. Elias Mashala na muuguzi kwenda nchini Marekani na watoto,” alisema Nyalandu.

 

Naye Mwakilishi wa Shirika la Samaritan’s Purse, Edward Morow, akizungumza kwa niaba ya Rais wa Shirika hilo, Frankline Graham, alisema imekuwa ni siku ya furaha kwao kuwaona watoto hao wakirejea nyumbani wakiwa wazima na wenye afya.

Meya wa Jiji la Arusha, Lazaro alisema kwa upande wake anamshukuru Mungu kwa muujiza wa kupatikana kwa safari ya watoto hao kwenda kutibiwa Marekani na hatimaye kurejea nchini wakiwa wazima.

Mama wa Sadia alisema mwanaye aliondoka na kitanda, leo amerudi akiwa anaweza kutembea, kula na anazungumza na hivyo anawashukuru Watanzania kwa sala na dua zao.

Naye mama wa Wilson, Neema Matemba, mbali na kushukuru, aliwasifu Wamarekani kwa kupata tiba nzuri kuliko ile inayopatikana Tanzania.

 

NJE YA KIA

Mara baada ya watoto, madaktari na wazazi kuondoka uwanja wa ndege, msafara uliekea katika kijiji cha Stemm, kilichopo eneo la Mbuguni, wilayani Arumeru, mahali ambako watoto hao wataangaliwa afya zao hadi leo.

Wakati wakielekea huko, baadhi ya barabara zilifurika mamia ya watu, wakiwamo wanafunzi waliosimama pembezoni mwa barabara wakiwa wameshika mabango yenye ujumbe wa kuwakaribisha wenzao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles