Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Chuo Kikuu cha St. Joseph kimezindua maonyesho ya ubunifu (Tan Tech 2018) ambapo wanafunzi wa chuo hicho wamepata nafasi ya kuonesha kazi mbalimbali walizobuni.
Maonyesho hayo yamefanika jijini Dar es Salaam leo Agosti 29, katika viwanja vya Mlimani City ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu Anthony Mavunde.
Akizungumza wakati wa maonyesho hayo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Burton Mwamila amesema uongozi wa chuo hicho umeamua kushirikiana na wanafunzi ili kuyapata tija zaidi maonesho hayo baada ya wanafunzi kufanya maonyesho kadhaa ya aina hiyo, peke yao.
[embedyt] https://www.youtube.com/watch?v=0h9ZSLA4YsU[/embedyt]
“Tumeamua kushirikiana na wanafunzi kuwaonesha Watanzania vipaji tulivyo navyo katika chuo chetu ila tu wanahitaji kuwezeshwa ili kuleta mapinduzi nchi inapoelekea katika Tanzania ya Viwanda na kuwapima ili kuona ni namna gani wanatumia elimu wanayopata darasani.
“Lakini pia, tumeamua kushirikiana na wanafunzi ili kuonesha watu kuwa chuo chetu kinatoa wahitimu waliowiva, wenye ubunifu wa hali ya juu na wana uwezo wa kujiajiri hivyo tunaiomba serikali iwape mazingira wezeshi ili mawazo yao yatumike katika kuendeleza sekta ya viwanda,” amesema.
Maonesho haya yatafanyika kwa siku tatu kuanzia leo Agosti 29 hadi Agosti 31 ambapo wageni watakaotembelea watapata nafasi ya kuona vitu mbalimbali vinavotengenezwa na wanafunzi hao lakini pia wataweza kuchangia damu.