Na Nora Damian, Mtanzania Digital
“Kwanza heshima yako kama inawezekana naomba siku nije Ikulu tuongee vizuri mimi na wewe,” anasema Emmanuel Mzena alipozungumza kwa simu na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa sherehe za kumpongeza katika siku yake ya kuzaliwa zilizofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa.
Emmanuel mwenye ulemavu na anayesoma kidato cha sita alisoma risala kwa niaba ya wanafunzi wenzake kitendo kilichomvutia pia Rais Samia ambaye alipopiga simu wakati sherehe hizo zikiendelea alizungumza naye.
Mwanafunzi huyo wakati akizungumza na Rais Samia alishindwa kujizuia na kutoa machozi huku akimuomba kukutana naye ombi ambalo Rais Samia alikubali na kuahidi kufanya ziara ya kutembelea shule hiyo.
“Nikiwa Dar es Salaam nitakuja kutembelea shule ya Benjamin Mkapa,” alisema Rais Samia.
Sherehe hizo za miaka 62 ya Rais Samia zilipambwa kwa matukio mbalimbali yaliyohusisha wanafunzi wasio na ulemavu na wale wenye ulemavu ambayo yalitafsiriwa kwa lugha ya alama na wanafunzi wenyewe.
Mathalani wimbo wa Taifa na ule wa kumpongeza Rais Samia kwa siku yake ya kuzaliwa uliimbwa kwa sauti kisha kwa lugha ya alama huku pia kukiwa na igizo lililoigizwa na wanafunzi viziwi.
Aidha kulikuwa na salamu zilizotolewa na wanafunzi kwa lugha mbalimbali zikiwemo Kichina na Kifaransa ambazo zote kwa pamoja zilipamba sherehe hizo.
TAALUMA
Mkuu wa shule hiyo, Deo Joseph, anasema ina wanafunzi 1,635 wakiwemo wa kike 719 na wa kiume 916 huku pia ikiwa inatoa elimu jumuishi ambapo ina wanafunzi viziwi, wenye ualbino, wenye uono hafifu na wenye ulemavu wa viungo.
Anasema kitaaluma shule hiyo inafanya vizuri kwani matokeo ya kidato cha sita 2021 wanafunzi wote walifaulu kwa asilimia 100 wakati kidato cha nne 2021 wamefaulu kwa asilimia 96.3.
“Tunashukuru kwa ujenzi wa madarasa nchi nzima na kuwezesha wanafunzi kusoma kwa amani na utulivu, tunashukuru kwa fedha za ujenzi wa madarasa mawili tumejenga na yamekamilika kwa ubora kabisa,” anasema Mwalimu Joseph.
Hata hivyo anasema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa chumba cha kupimia viziwi kwa ajili ya kujua kiwango cha uziwi ili kumsaidia mwanafunzi ipasavyo.
“Tunaomba kujengewa maktaba na ukumbi wa mikutano ambao utatusaidia wakati wa mvua na pia wakati wa mitihani, tayari michoro ipo na eneo la ujenzi lipo,” anasema.
Pia wanaomba kupatiwa gari ili kurahisisha huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa kuwa ni changamoto wakati maradhi yanapowafika sambamba na kujengewa bweli kwa ajili ya wanafunzi hao.
Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ambaye alilishwa keki kwa niaba ya Rais Samia, anasema sekta ya elimu iliongezewa bajeti ya Sh bilioni 368 zilizotumika kuboresha miundombinu katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo kujenga shule shikizi 3,000, shule za sekondari 12,000, mabweni 50 ya wanafunzi wa kike na kumbi 15 katika vyuo vya elimu.
“Rais Samia ameleta matumaini makubwa na kulifanya taifa lizidi kuendelea mbele kwa kuwaunganisha Watanzania na kuwa wamoja,” anasema Profesa Mkenda.
MAJIBU YA CHANGAMOTO
Rais Samia ameahidi kutatua changamoto zinazoikabili shule hiyo ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira mazuri.
“Kwa ujumla mambo ndani ya sekta ya elimu ni mengi, baada ya kujenga madarasa kinachofuata ni kuajiri walimu. Shule za msingi bado kuna uhitaji mkubwa wa madarasa…kazi sekta ya elimu ni kubwa lakini tutaendelea kuifanya,” anasema Rais Samia.