NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM
MEYA wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Omary Kumbilamoto, amesema katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba mwaka huu wanatarajia zaidi ya wanafunzi 20,000 watafaulu na kwenda sekondari kutokana na maandalizi waliyoyafanya.
Katika mtihani wa mwaka jana halmashauri hiyo ilifaulisha wanafunzi 21,400 na kushika nafasi ya nne kitaifa na nafasi ya pili kimkoa huku ikiwa na wastani wa ufaulu wa asilimia 95.59 ikilinganishwa na asilimia 92.46 za mwaka juzi.
Akizungumza jana wakati wa mahafali ya darasa la saba katika Shule ya Msingi Bunge, Kumbilamoto alisema wanafunzi 25,000 wanatarajia kufanya mtihani huo mwaka huu na kwamba tayari wamekamilisha maandalizi yote.
“Tunatarajia kupata matokeo mazuri kama mwaka jana kutokana na juhudi za ufuatiliaji ambazo zimekuwa zikifanywa na idara ya elimu msingi, na hata katika mitihani ya kujipima wanafunzi wengi walifanya vizuri,” alisema Kumbilamoto.
Meya huyo aliwataka wazazi kuwaandaa vyema watoto wanaotarajiwa kufanya mtihani huo kwa kuwatia moyo kwani kushindwa mtihani kunachangiwa pia na maandalizi duni kutoka kwa wazazi na walezi.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bunge, Radhia Mfalingundi, alisema kiwango cha taaluma shuleni hapo kimekuwa kikipanda mwaka hadi mwaka na kwamba mwaka jana wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 238 na kati yao waliofaulu ni 232 sawa na asilimia 97.4.
Hata hivyo alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hasa uchakavu wa majengo, miundombinu ya umeme, upungufu wa vifaa vya kufundishia masomo ya sayansi, samani za ofisi na darasani na utoro unaochangiwa na ushirikiano mdogo wa wazazi.
Shule hiyo yenye wanafunzi 2,480 wakiwemo wavulana 1,255 na wasichana 1,225 ilianzishwa mwaka 1957 ikiwa chini ya Wakoloni na mwaka 1963 ilikabidhiwa rasmi kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kupewa jina la Bunge.