Hadija Omary, Lindi
Jumla ya wanafunzi 11,808 waliohitimu elimu ya msingi mwaka huu katika shule mbalimbali mkoani Lindi, wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2019.
Akitangaza matokeo hayo jana, Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Rehema Madenge, amesema wanafunzi waliofanya mtihani huo walikuwa 19,046 ambapo wavulana walikuwa 8,790 na wasichana 10,256.
“Kati ya hao waliofaulu walikuwa wanafunzi 13,074 sawa na asilimia 68.71, wavulana wakiwa 6,286 na wasichana 6,788 huku wanafunzi 11,808 sawa na asilimia 90 wakichaguliwa na wavulana wakiwa 602 na wasichana 664.
“Aidha, kati ya wanafunzi 13,074 waliofaulu wanafunzi 1,266 sawa na asilimia 9.68 hawakuchaguliwa kutokana na sababu mbalimbali za miundombinu ikiwamo uhaba wa madarasa,” amesema.
Pamoja na mambo mengine, Madenge pia alitumia fursa hiyo kuwataka wakurugenzi watendaji wa mkoa huo kuhakikisha wanafunzi wote waliokosa nafasi kwa sababu ya ukosefu wa miundombinu wanaanza masomo ifikapo Februari 15, mwakani.