UKITAKA kuzungumzia muziki wa Hip Hop nchini Marekani kwa sasa, hawezi kumuacha nyota wa muziki huo Kendrick Lamar ambaye anaonekana kufanya vizuri na kuwapoteza wakongwe.
Siyo kazi nyepesi kuingia kwenye muziki wa Hip Hop na kukubalika haraka, ni lazima kichwa kifanye kazi ili kuweza kuandaa mistari itakayowafanya mashabiki wengi wakuelewe.
Haikuwa kazi kubwa kwa Kendrick kuwashawishi mashabiki duniani kutokana na aina ya muziki wake ambapo mashabiki wengi walianza kusema kuwa 2 Pac Shakur amerudi tena duniani.
Walisema hivyo kutokana na muziki wa msanii huyo kufaninishwa na marehemu 2 Pac. Hata hivyo ilikuwa kazi ngumu kwa wasanii wakongwe kumkubali msanii huyo mapema ila ilibidi wakubaliane naye kwa kuwa ana kipaji cha aina yake.
Siku zote muziki wa Hip Hop unahitaji mistari ambayo inaweza kumfanya msikilizaji afikirie jambo kwa undani zaidi, ndiyo maana wasanii wenyewe inakuwa kazi kukubalika kama mistari yao inakuwa ya kawaida.
Hii ni tofauti na muziki wa RnB ambapo wasanii wake hawana ujanja sana wa kutunga mistari ya kuumiza vichwa, hasa ujanja wao ni pale wakiwa jukwaani, jinsi wanavyocheza na sauti zao zinaweza kuwavuta mashabiki wengi.
Kwa upande wa Marekani kwenye muziki wa RnB huwezi kumuacha mkali wao Chris Brown, ambaye amekuwa ni kipenzi cha wanawake hasa kutokana na uwezo wake wa kuimba na kucheza, pia ana idadi kubwa ya mashabiki wa kiume.
Kwa upande wa muziki wa Hip Hop, Lamar alianza kuitwa 2 Pac tangu mwaka 2013 ambapo alionesha uwezo wake wa kuandika mashairi, lakini hakuwa na idadi kubwa ya mashabiki kama ilivyokuwa mwaka 2014 ambapo alifanikiwa kuchukua tuzo nyingi kwenye tuzo za Black Entertainment Televisheni (BET).
Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuingia kwenye tuzo hizo lakini alifanikiwa kuibuka kinara kwa kuondoka na tuzo nyingi kuliko msanii mwingine, alipata tuzo hizo kutokana na kuwa chipukizi, kufanya video kali, wimbo bora wa mwaka, kolabo bora na mtumzi bora wa mwaka.
Hali hiyo ilimpa jina kubwa na ndipo akaanza kujiita ‘King of Hip Hop’ lakini ilikuwa ni ngumu wasanii wenzake wa Hip Hop kukubali kuwa Lamar ni mfalme, ila walimkubali taratibu kutokana na kazi zake mbalimbali baada ya tuzo hiyo.
Msanii huyo aliumaliza mwaka 2015 kwa kuzidi kuwachanganya wasanii wenzake kwa kutangazwa kuwa msanii pekee wa Hip Hop ambaye ametoa albamu bora kwa mwaka huo ambapo ilijulikana kwa jina la ‘To Pimp a
Butterfly’.
Hapo ndipo baadhi ya wasanii wakubwa kama vile The Game, P. Didy na wengine wengi kumkubali msanii huyo na kusapoti jina lake ambalo alijipatia la King of Hip Hop. Msanii kama The Game ana jina kubwa duniani hasa katika muziki huo wa Hip Hop, wakati huo P.Didy akiwa katika orodha ya wasanii wa muziki huo ambao ni matajiri
wakubwa duniani, lakini wote wamemkubali msanii huyo kutokana na kazi anazofanya na kufananishwa na 2 Pac.
Mwaka jana, msanii huyo alitamba na nyimbo zake nyingi kama vile Alright, The Blacker The Berry na These Walls.
Mbali na hapo alitamba na Swimming Pools, ambao aliachia mwaka 2012 na kumpa jina kubwa katika muziki huo.