Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Mazingira rafiki ya biashara yaliyowekwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, yamechangia kuongezeka kwa meli katika Bandari ya Dar es Salaam na kuongeza fursa ya usafirishaji wa mizigo nje ya nchi.
Hayo yamezungumzwa leo Desemba 20, 2023 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Wamiliki wa Malori Nchini (TAMSTOA), Chuki Shabani wakati wa mkutano mkuu wa nne wa mwaka uliyowakutanisha wadau mbalimbali katika sekta ya usafirishaji.
Amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia ni sikivu kwani yapo mambo mengine ambayo yalikuwa yakiwakumba imeweza kuyatatua kwa wakati.
Aidha amesema maroli yao yanabeba mizigo ya watu wa nchi za nje hivyo ukamataji unaoendelea hasa katika Wilaya ya Temeke unakwamisha ufanyikaji wa biashara hiyo kwa wakati.
“Tusimkatishe tamaa Rais wetu kwa juhudi hizi anazozionyesha, tuendelee kushirikiana kuhakikisha mazingira rafiki ya ufanyaji wa biashara nchini yanaendelea kuwa bora zaidi,” amesema Shabani
“Sisi maroli yetu yanabeba mizigo kupeleka nchi za nje, trafiki unapoyakamata na kukaa nayo zaidi ya saa tano kisa unamdai dereva faini ya Sh 50,000 ambayo kwa wakati huo anakuwa hana.
“Ni bora kuachia gari iondoke kupeleka mzigo hadi ikirudi kuliko kuikamata kwa saa zaidi ya tano ambazo angezitumia kufika hata Mbeya, tunaiomba serikali kupitia Jeshi la Polisi kutusaidia kutatua changamoto hii kwa kuwapatia elimu watendaji,” amesema.
Ametaja changamoto nyingine kuwa ni usalama wa mizigo na madereva katika nchi za Congo na Zambia kutokana na kuwa tishio katika utekelezaji wa biashara ya usafirishaji wa mizigo.
“Hali hii imesababisha kuwa na matukio ya mara kwa mara ya utekaji wa magari ya mizigo inayosababisha hasara kwa wamiliki na madhara kwa madereva mfano kujeruhiwa na wengine kuuawa, ila tumeambiwa jambo hili linafanyiwa kazi,” amesema.
TAMSTOA wameiomba serikali kutatua changamoto ya kukamata kwa maroli inayochangia kuchelewesha mizigo inayosafirishwa kwenda nje ya nchi.
Akijibu changamoto ya kukamatwa kwa maroli, Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Barabara kutoka Wizara ya Uchukuzi, Andrew Magombana amesema watakutana na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ili kutatua jambo hilo kwa wakati.
“Tutakutana na wenzetu wa Tarura pamoja na Tanroads ili kuhakiksha changamoto hii ya kamatakamata ya maroli inatatuliwa kwa wakati, tuunaendelea na vikao nyetu vya kazi mapema tu tunalitatua jambo hilo na mwenzetu wanaendelea na kazi kama kawaida,” amesema Magombana.
Amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia ipo pamoja na wamiliki wa maroli nchini hasa katika kuonesha nia dhabiti ya kusikiliza changamoto zao zinazowakabili na kuweza kuzitatua.
Magombana amesema kwa sasa kuna sheria rasmi kuhusu maslahi ya kundi hilo, hivyo amewataka madereva kwa umoja wao waifuate.