27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wamiliki wa makampuni waijia juu Bandari

Dk.John Magufuli*Watoa masharti mazito, wadai kudhalilishwa

TUNU NASSOR NA AMANI MAKALA (RCT), DAR ES SALAAM

SAKATA la kufungiwa kwa makapuni 283 kutoa huduma ya mizigo bandarini (Clearing and Forwarding Agents), limechukua sura mpya ambapo wamiliki wake wamekutana na kutoa masharti kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Pamoja na hatua hiyo, wamemuomba Rais Dk. John Magufuli kuhakikisha anatumbua majipu zaidi kumshughulikia Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mhandisi Aloyce Matei ambaye anadaiwa kukusanya ‘dispatch’ zote za malipo kwenye bandari kavu (ICDs).

Licha ya hatua hiyo, pia wamiliki hao wa makampuni wameunda Kamati Maalumu inayoshirikisha wadau wa bandari pamoja na Serikali ambayo leo inaanza kufanya vikao vyake vitakavyobaini uhalali wa kufungiwa kampuni 283 za uondoshaji wa mizigo bandarini.

Akizungumza jana katika mkutano wa wadau wa bandari, Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Steven Ngutunga, alisema vikao hivyo vimekuja baada ya wao kuwasilisha mapendekezo ya kuomba tume huru itakayofanya uchunguzi kubaini chanzo cha tatizo hilo.

Ngutunga alisema kamati hiyo itashirikisha wajumbe kutoka serikalini, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), vyama vya wadau wa bandari ambao ni TAFFA, Chama cha Mawakala wa Meli (TASAA), Chama cha Wasafirishaji kwa njia ya Barabara (TATOA), Chama cha wenye Bandari Kavu (CIDAT) na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA).

Alisema wanashangazwa namna wanachama wao wanavyoonewa pamoja na kulipa kodi zote zinazohitajika kupitia benki.

“Sisi TAFFA tutawasilisha ushahidi tulionao, unaoonyesha wanachama wetu walivyokuwa wakilipa kupitia benki mbalimbali kwa kuwa wamiliki wa bandari kavu wana kila aina ya vielelezo vya kutosha,” alisema Ngatunga.

Alisema wana ushahidi wa benki zilizolipwa kwa hundi na baadaye kubaini kwamba hundi hizo zilitumika kulipia kampuni nyingine.

Kutokana na hali hiyo, wameiomba Serikali kuzifungulia kampuni hizo ziweze kuendelea na kazi zake wakati vikao hivyo vikiwa vinaendelea kutafuta usahihi wa suala hilo.

“Tunamuomba Rais Magufuli kuendelea kutumbua majipu TPA kwa kuwa bado yapo kuanzia kwa mkurugenzi aliyepo sasa hadi kwa wakusanya ushuru katika ICDs,” alisema Ngutunga.

Rais huyo wa TAFFA alisema wanashangazwa na uongozi wa TPA kukusanya nyaraka mbalimbali zilizotumika kwa ajili ya kuruhusu uondoshaji wa makontena.

“Katika kikao tulichofanya na uongozi wa TPA. mkurugenzi wake alikiri kupotea kwa baadhi ya nyaraka zikiwemo ‘Dispatch’ alizoziagiza kuchukuliwa katika ICDs,” alisema Ngutunga.

Kutokana na hali hiyo, wameiomba Serikali kutoa tamko la kuwasafisha baada ya kuitwa wezi, kwani hivi sasa wanashindwa kufanya kazi na wadau wanashindwa kuwaamini.

Alisema hatua ya kutangazwa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari na kuambiwa ni wezi imewafedhehesha na kuwaumiza, kwani ni jambo lisilokubalika, hasa katika kujenga uchumi wa taifa.

“Ni vema Serikali ikatoa tamko litakaloweza kutusafisha baada ya kutangazwa dunia nzima kuwa sisi ni wezi wakati wanaofanya udanganyifu ni benki na TPA,” alisema Ngutunga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Smart Forwarders, Radish Kamaniya, alidai kwamba alilipa Sh milioni 40 kupitia benki na kupewa nyaraka zote ikiwamo stakabadhi.

“Nilifanya malipo benki kwa hundi, lakini baada ya mwaka mmoja na nusu niliambiwa sijalipa na kutakiwa kulipa tena. Ila nilipofuatilia ilibainika hundi imelipia makampuni mengine,” alisema Kamaniya.

 

MWAKILISHI WA SERIKALI

Akijibu hoja za mawakala hao wa forodha, mwakilishi wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa, Raymond Mbilinyi, alisema wamesikia mapendekezo hayo na yatafanyiwa kazi.

“Pamoja na kuyashughulikia mapendekezo hayo, niwaombe wadau wote wa bandari kumuunga mkono Rais John Magufuli katika jitihada zake za kuimarisha uchumi,” alisema Mbilinyi.

KAULI YA BANDARI

Kutokana na madai hayo ya TAFFA, MTANZANIA ilimtafuta Mkuu wa Mawasiliano wa TPA, Janeth Luzangi, ambaye alikiri baadhi ya hoja za mawakala hao ikiwamo ya kupotea kwa ‘dispatch’  kwenye bandari kavu.

“Ni kweli kuna upotevu wa ‘dispatch’, na hili lilifanywa na baadhi ya wafanyakazi ambao si waaminifu kwa kushirikiana na baadhi ya wafanyabiashara, na tayari tumewasimamisha kazi wale wote waliohusika,” alisema Janeth.

Alisema kampuni 127 zimelipa fedha zinazodaiwa na mamlaka hiyo na tayari zimeshafunguliwa ili ziweze kuendelea na kazi kupitia bandari.

Akizungumzia tuhuma za kutumia udhaifu wa mkurugenzi mkuu ambaye ni mhandisi kitaaluma kuwabana wafanyabiashara, msemaji huyo alisema suala hilo halina ukweli.

“Ni kweli mkurugenzi ni mhandisi, hana taaluma ya biashara, lakini ana uzoefu na masuala haya kwa muda mrefu,” alisema.

Februari 10, mwaka huu TPA ilitangaza kuyazuia makampuni 210 kupitisha mizigo yao bandarini pamoja na washirika wake (ICS’s, CF’s na TICTS).

Uamuzi huo wa bandari ulitolewa miezi michache tangu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipofanya ziara bandarini hapo na kubainika upotevu wa makontena zaidi ya 2,000 kupitishwa bila kulipiwa kodi kwa mujibu wa sheria.

Taarifa iliyotolewa na Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Fred Liundi, ilieleza kuwa uamuzi huo umechukuliwa dhidi ya makampuni hayo baada ya kushindwa kuwasilisha vielelezo vya malipo kama walivyotakiwa na TPA.

Mbali na hilo, pia wamiliki wa kampuni hizo walishindwa kufika bandarini kupokea nyaraka kadhaa kuhusu madeni wanayodaiwa na TPA kwa mujibu wa mizigo yao waliyopitisha bandarini hapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles