29.9 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Wamiliki wa Clouds waamriwa kufika mahakamani kusikiliza shauri la wafanyakazi

Na Imani Nathaniel, Mtanzania Digital

Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi Dar es Salaam imewataka wamiliki wa Kampuni ya Clouds Media Group kufika mahakamani hapo Julai 17, 2024, kusikiliza shauri la madai namba 12076 la mwaka huu.

Amri hiyo ilitolewa na Jaji Biswalo Mganga wakati shauri hilo lilipotajwa kwa ajili ya maandalizi ya kusikilizwa. Shauri hilo lilitokana na uamuzi uliotolewa Aprili 16, 2024, na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi wa Mgogoro ya Kikazi (CMA).

Inadaiwa kuwa Aprili 4, 2021, wafanyakazi 16 wa Clouds Media Group, wakiwemo Issa Maeda na wenzake 15, walifutwa kazi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni mahitaji ya kiutendaji. Wafanyakazi hao waliwasilisha mgogoro wao kwenye CMA Mei 8, 2021, wakidai kuwa walifutwa kazi isivyo halali.

Walalamikaji walikuwa wakiiwakilishwa na wakili Godfrey Lugomo, huku mlalamikiwa akiwakilishwa na mawakili Alex Mushumbusi na Lujjaina Mohamed. Pande zote mbili ziliwasilisha maelezo ya awali kupitia mawakili wao, na baadaye hoja zikaainishwa, zikiwemo endapo kulikuwa na sababu za msingi za kuachishwa kazi, endapo taratibu zilifuatwa, na stahiki za kila upande.

Katika uamuzi wake, Tume ilizingatia ushahidi uliotolewa na mashahidi wote watano pamoja na vielelezo vilivyowasilishwa. Tume iliona kuwa walalamikaji walifutwa kazi kwa mahitaji ya kiuendeshaji baada ya kampuni kuyumba kibiashara na kiuchumi kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19. Mlipuko huo uliathiri biashara nyingi, na makampuni mengi kusitisha mikataba ya matangazo kwenye redio na televisheni, hali iliyosababisha mauzo kushuka kwa asilimia 50 na kuathiri mapato ya kampuni kwa kiwango kikubwa.

Baada ya uchunguzi wa kina, Tume ilihitimisha kuwa walalamikaji hawakustahili malipo mengine yoyote zaidi ya yale waliyopewa, kwani walipunguzwa kazi kwa sababu na taratibu halali kisheria. Walipokea stahiki zao zote kwa mujibu wa sheria na makubaliano yaliyofikiwa na Clouds Media Group wakati wa mchakato wa kuwapunguza kazi.

Hata hivyo, walalamikaji walikata rufaa wakipinga uamuzi huo wa CMA Kanda ya Dar es Salaam, na kuiomba Mahakama ya Divisheni ya Kazi kuangalia upya uamuzi huo ili wapate stahiki zao kisheria. Shauri hilo linasubiri kusikilizwa tena Julai 17, 2024.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles