Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema itawaondolea huduma na kuwachukulia hatua za kisheria watu waliosajili laini zao kwa vitambulisho vya watu wengine au kwa kutumia kitambulisho tofauti.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya baadhi ya watu kufungiwa huduma za simu kutokana na kutosajili laini zao za simu kwa alama za vidole kwa mujibu wa sheria.
“Katika kujiridhisha kuwa waliosajili laini zao za simu wametumia vitambulisho sahihi, TCRA kwa kushirikiana na watoa huduma itafanya zoezi la kuhakiki laini zote zitakazokuwa zimesajiliwa ili kuwaondoa wale waliosajili laini zao ama kwa kutumia vitambulisho vya watu wengine au kwa kutumia vitambulisho tofauti sambamba na kuwachukulia hatua za kisheria.
“Ikumbukwe kwamba kusajili laini ya simu kwa kutumia kitambulisho cha mtu mwingine ni kosa sanjari na kupewa laini iliyosajiliwa na mtu mwingine,” imesema taarifa ya Mamlaka hiyo.
Pamoja na mambo mengine, TCRA imesema waombaji wapya wa laini za simu wataendelea kusajiliwa muda wote kwa kutumia kitambulisho cha taifa na kuhakikiwa kwa alama za vidole ambapo huduma hiyo ni endelevu.