28.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 3, 2024

Contact us: [email protected]

Waliotangaza ajira feki waanza kuhojiwa

IGP Mangu
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Mangu

NA FREDERICK KATULANDA, MWANZA

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limeanza uchunguzi kwa kuwahoji viongozi watatu wa mradi wa kimataifa unaohusika na masuala ya Ukimwi ambao wanadaiwa kutangaza ajira feki zaidi ya 1,500.

Mbali na hilo, pia wamezuiwa kusafiri nje ya Mkoa wa Mwanza bila idhini ya Polisi.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, zilieleza wasimamizi wakuu wa mradi wa kimataifa wa Ukimwi ambao wamekuwa wakijitambulisha chini ya Taasisi ya Popular Culture and Sport Project (PCSP), mbali na kuhojiwa, pia wametakiwa kuthibitisha uwezo wa kutoa ajira hizo.

Kuhojiwa kwa viongozi hao na polisi kumeibuka baada ya gazeti hili Juni 24 kuandika kuhusiana na utata wa ajira hizo.

Waliohojiwa na Polisi ni Mratibu Mkuu, George Mashiba, Meneja Rasilimali Watu, Frederick Tingatinga pamoja na Mhasibu aliyetambulika kwa jina moja la Mariam.

“Ni kweli tumeanza uchunguzi wa suala hili, tumewahoji wahusika…, siwezi kueleza zaidi masuala mengine ila nichukue nafasi hii kuwaomba wale wote ambao wanatambua kuwa ni victim (waathirika) wa ajira hizi wafike ofisini kwangu,” alieleza Kamanda.

Utata wa Taasisi waibuka

Taasisi ya Mwanza Popular Culture and Sport Programme (PCSP) imeibuka na kusema jina la asasi yake limetumika visivyo kwa vile ajira hizo zinatolewa na The Executive Committee for the International Project HIV and AIDS.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Andrea Mabagala ameibuka na kudai ameshtushwa na kusikia jina la asasi yake likihusishwa na utoaji wa ajira na kubainisha kuwa Taasisi inayojulikana kama Mwanza Popular Culture and Sport Programme (PCSP) ilisajiliwa Baraza la Michezo Mei 6 mwaka 2003 na baadaye Juni 5 mwaka 2014 asasi hiyo ilisajiliwa kama shirika lisilo la kiserikali (NGO) na kubadilika jina na kuwa Popular Culture, Youth and Sport Organization (PCYSO-Tanzania).

Mabagala, ambaye ni Ofisa Utamaduni Mstaafu wa Michezo na Meneja Mkuu wa PCYSO Tanzania, alidai hata katika mfumo wa NGO yake hahusiki na utoaji ajira na kubainisha kuwa anawafahamu wanaohusika na ajira hizo ambao alikiri wapo jengo moja na mara kadhaa wamewahi kukutana nao na kuwaonya kutojihusisha na jina la asasi yao.

“Tulipopata taarifa hizi tuliamua kuwaita haraka kueleza jina la asasi inayotajwa kuhusika na hizo ajira ni letu, lakini sisi hatuhusiki na utoaji wa ajira, kazi yetu ni masuala ya michezo. Ninachoweza kueleza ni kuwa katika ofisi hii tulipo kuna watu ambao wamekuwa wakihusika na masuala hayo,” alisema.

Nafasi ambazo zimekuwa zikitangazwa kila mara na kupata waombaji wapya kati ya 50 hadi 150 kwa kipindi cha wiki tatu, wamekuwa wakitozwa ada ya Sh 30,000 ya kufanyiwa usaili, huku wengine wakitozwa zaidi ya kiasi cha Sh 150,000 hadi 500,000 kwa ajili ya kupewa kipaumbele zaidi na kuwekwa kwenye orodha ya waliokubaliwa kuajiriwa kwa kisingizio cha ajira chache.

Katika usaili huo, imebainika kuwa pamoja na kutozwa Sh 30,000 za ada ya usaili, pia wamekuwa wakitozwa Sh 5,500 kwa ajili ya kupatiwa kitambulisho, kupigwa picha kwa ajili ya kufungulia akaunti benki, lakini licha ya hayo yote, watu hao wamekuwa wakiendelea kusota bila ajira kwa muda mrefu sasa tangu mwaka 2011.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Nasikitika kuwa mwathirika wa hili tatizo. Kuna rafiki yangu ambaye kahitimu UDOM ambae yupo kwenye ofisi hiyo kwa zaidi ya miezi miwili. Alinipigia cm nakuniambia BOSI yake anaejiita chief kamwambia kuna nafasi mbili za kazi hivyo alinipigia cm nakuniomba sana nisiizipoteze nafasi hizo. Aliniambia interview ilishakamilika na hivyo nafasi hizo zilibakishwa kwa ajili ya wakubwa kuweka watu wao hivyo zinatakiwa laki mbili. Pasipo kuchunguza niliamua kusafiri hadi Mwanza nakufanya kama nilivyoelekezwa. Baada ya yakuwa nimeshalipa pesa nakujua jina la kampuni niliamua kuingia kwenye mtandao ili kupata taarifa zao, na badala ya kupata taarifa zao nzuri nilikutana scandal zao zilizoandikwa JamiiForum na kesho yake niliamua kumuuliza kijana aliyeniita. Hakuweza kunipa majibu yanayojiridhisha na hivyo ilibidi nisafiri tena hadi Mwanza na kukutana na CHIEF wa kampuni hilo na kumuuliza maswali ambayo hakuweza kuyajibu pia, nilimuuliza. Kwa nini kampuni yako haina hata blog? Taarifa sisi waajiriwa tutazipata wapi? Pia kampuni yako ina miaka minne mnaajiri tu bila wazungu kufika? Kijana aliyeniunganisha nachief nimeshamuomba anirudishie pesa yangu kwani ndiye niliyemkabidhi mkononi na yeye akampelekea chief tapeli la sivyo jtatu namvuta polisi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles