Na ELIYA MBONEA -MONDULI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Arusha, imeagizwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watu wanaodaiwa kutafuna Sh milioni 448.9 za mradi wa Machinjio ya Manyara Ranch wilayani Monduli mkoani hapa.
Agizo hilo lilitolewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo wakati wa ziara yake ya kutembelea mradi huo wa machinjia ya kisasa ndani ya shamba lenye ukubwa wa ekari 44,930.
Alikuwa ameongozana na Mbunge wa Jimbo hilo (Chadema), Julius Kalanga, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo (Chadema), Isack Joseph na viongozi wengine.
Gambo alishangazwa kuona mradi huo ulioanza mwaka 2009 ukiwa haujakamilika wakati fedha zilikwisha kutolewa.
Alisema zaidi ya Sh milioni 448.9 zilikwisha kutolewa kwa ajili ya gharama za ujenzi ikiwamo jengo la machinjio zaidi ya Sh milioni 223.5, ununuzi wa vifaa vya kisasa.
“Fedha zilizotolewa na wafadhili Shirika la Misaada la Kimataifa la Marekani (USAID), kupitia Shirika la African Wildlife Foundation (AWF).
“Fedha hizo zimeliwa na wachache wakiwamo wa Wizara ya Mifugo na Kilimo. Hili hatutalivumilia,” alisema Gambo na kuongeza:
“TAKUKURU mnapaswa kuchukua hatua kwa kuwasaka wote waliohusika kukwamisha huu mradi, wafikisheni katika vyombo vya sheria wakajibu tuhuma zao.
‘’Lazima waliokula fedha za wafadhili wanapaswa kukamatwa mara moja na hiyo nawaachia TAKUKURU ndani ya siku chache zijazo, nahitaji majibu kuwa wamekamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka yao’’.
Meneja wa AWF, Fidelis ole Kashe, alilitaja lengo la kujengwa machinjio hiyo kuwa ni kupanuaa wigo wa vyanzo vya mapato yanayotokana na kuuza mifugo na nyama bora katika kiwanda.
Alisema kiwanda hicho cha machinjio kililenga kutoa soko la kuuza mifugo na nyama kwa vijiji vinavyozunguka machinjio hiyo ikiwamo ajira itakayotolewa kwa wananchi hususan kwa jamii zilizo jirani.
“Upungufu uliopo katika mradi huo ni kutolewa fedha nyingi lakini hadi sasa mradi umeshindwa kukamilika, kukosekana kwa mwekezaji, vifaa vilivyotumika kujenga havina ubora,” alisema Kashe .