24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Waliokiri kutakatisha fedha waingiza Sh bilioni 6.5

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

WATUHUMIWA zaidi ya sita wa makosa ya uhujumu uchumi, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Benki M (Tanzania), Sanjeev Kumar (63), wamekiri makosa yao kwa nyakati tofauti na kulipa zaidi ya Sh bilioni 6.53.

Washtakiwa hao walikiri makosa yao jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya mahakimu watatu tofauti, baada ya kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuhusu kiasi cha fedha watakachorejesha.

Kwa upande wake, mshtakiwa Kumar ameamriwa kulipa fidia ya zaidi ya Sh bilioni 6 na faini ya Sh milioni 2 baada ya kukiri.

Kumar ametakiwa kuilipa fidia hiyo ndani ya miezi 24 na hadi sasa ameshalipa Sh milioni 690.

Akisoma adhabu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi, alisema katika mashtaka mawili, mshtakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh milioni moja kwa kila kosa. 

Alisema pia mshtakiwa atatakiwa kulipa fidia ya Sh 6,039,103,579 kwa miezi 24, kwamba kila mwezi atalipa Sh milioni 222.8.

Hati ya kusafiria ya mshtakiwa huyo itabaki katika Ofisi za DPP na safari zake zote zitafuatiliwa na ofisi hiyo. 

Wakili wa Serikali, Jackline Nyantori alidai kuwa wameingia makubaliano na mshtakiwa huyo baada ya kukiri kosa la kuisababishia serikali hasara, hivyo wameamua kuondoa mashtaka ya kughushi, kutakatisha fedha, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuwasilisha nyaraka za uongo.

Akisoma mashtaka mapya, Jackline alidai katika shtaka la kwanza, Januari 20, 2016 mshtakiwa huyo akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki M Tanzania, kwa vitendo vyake alivyovifanya aliisababishia Serikali kupata hasara ya Sh 6,039,103,579.

Katika shtaka la pili, mshtakiwa anadaiwa Januari 20, 2016 akiwa Dar es Salaam, kwa njia ya ulaghai ndani ya Benki M Tanzania akijua ni udanganyifu, alijipatia Dola za Marekani 287,000.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, aliyekuwa akishtakiwa pamoja na aiiyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake wanne, amekiri makosa ya kusababisha hasara ya Sh bilioni 1.1.

Mahakama imemwamuru kulipa faini ya Sh milioni nne na fidia Sh 293,446,400.23 kama walivyokubaliana na DPP.

Mshtakiwa akishindwa kulipa faini hiyo ataenda jela miaka 20. Amelipa.

Mdege alikiri jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salum Ally baada ya Jamhuri kuifahamisha mahakama kwamba mshtakiwa huyo aliandika barua ya kuomba msamaha kwa DPP na wakaingia makubaliano.

Kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladislaus Komanya aliwasomea washtakiwa wote mashtaka 50 badala ya 100 yaliyokuwa yakiwakabili awali.

Aliwataja washtakiwa kuwa ni Maimu, Meneja Biashara wa Nida, Avelin Momburi na Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Ndege, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Komanya alidai washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 50, yakiwemo ya kutumia nyaraka kumdanganya mwajiri, kughushi, kutoa nyaraka za uongo, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Sh 1,175,785,600.93 kwa Nida.

Washtakiwa wote walikana mashtaka isipokuwa Ndege alikiri shtaka la kwanza la kujihusisha na genge la uhalifu na shtaka la kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni moja.

Baada ya kukiri, mahakama ilimtia hatiani na upande wa Jamhuri uliomba apewe adhabu kulingana na makubaliano, mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, kaomba msamaha, itasaidia kupunguza msongamano gerezani.

Katika shtaka la kusababisha hasara, inadaiwa Maimu, Ndege na Ntalima kati ya Julai 19, 2011 na Agosti 31 mwaka 2015 katika maeneo tofauti ya Dar es Salaam kwa udanganyifu walisababisha hasara jumla ya Sh 1,175,785,600.93 dhidi ya Nida.

Nao mfanyabiashara David Mudi na wenzake wanne, wamehukumiwa kulipa fidia ya Sh milioni 40 baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya uhujunu uchumi kwa kujihusisha na nyara za Serikali bila kibali.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mohamed Salum Mohamed, Mustapha Bakari, Salum Wakili na Shabani Haji.

Washtakiwa hao walipewa adhabu hiyo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Janet Mtega.

Mbali na adhabu hiyo, washtakiwa hao walipewa adhabu ya kifungo cha nje kwa sharti la kutofanya kosa hilo tena na washirikiane na Serikali kutoa taarifa za watu wengine wanaojihusisha na makosa kama hayo.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wanakabiliwa na kosa moja kuwa kati ya Novemba mosi hadi 16 mwaka 2015, Zanzibar na Dar es Salaam, wote walijihusisha na usafirishaji wa kobe 201 wenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 40 bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Wakati huo huo, mshtakiwa Priscus Shirima anayeshtakiwa kwa uhujumu uchumi atalipa fidia ya Sh milioni 153 kwa miezi mitatu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles