NA MARY MWITA
BAADHI ya wasichana waliokimbia wakati wakilazimishwa kukeketwa ili wapatiwe wachumba kwa mujibu wa mila na desturi za kabila zao wamedai wametimiza ndoto zao za kupata elimu.
Walisema kukimbia ukeketaji kumewapa mwanga wa maisha na kutimiza ndoto zao za kuishi maisha bora na kudai bado kuna ukatili wa watoto wa kike katika jamii za wafugaji.
Mkazi wa Arumeru, Riziki Meijo alisema akiwa mmoja waathirika wa ukatili wa ukeketaji alikombolewa na Shirika lisilo la kiserikali la Health Integrated Multisectoral Development (HIMD) na tayari amewezeshwa kufanya shughuli za kiuchumi.
Alisema ukeketaji ni hatari na baadhi ya wasichana waliofanyiwa ukatili huo wameathirika kisaikolojia.
Mkurugenzi Mtendaji wa HIMD, Mackrine Rumanyika alisema baadhi ya jamii bado zinafanya ukeketaji na kutaka mamlaka husika kuchukua hatua stahiki kudhibiti ukatili huo.
Alisema wasichana zaidi ya 100, wamekimbilia na kupewa msaada katika shirika hilo.
Mackrine alisema wanasaidia wasichana wanaokimbia kwa kuwapatia elimu hadi vyuo vikuu na kuwa wamekuwa msaada kwa familia zao na kuwa jamii bora kwa wasichana wa jamii zao.
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 imeendelea kusimamia masilahi mapana ya mtoto bila kubagua jinsi, na sera ya elimu ya mwaka 2015 imekataza kila aina ya unyanyasaji wa mtoto wa kike na kutambua misingi ya haki na usawa kwa watoto wa kike na wa kiume.