BAMAKO, MALI
VIONGOZI wa mapinduzi ya kijeshi huko Mali wameuambia ujumbe wa wapatanishi wa Magharibi mwa Afrika kuwa wanataka kusalia madarakani kwa miaka mitatu ya kipindi cha mpito.
Wapatanishi kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (Ecowas) walitumwa Mali mwishoni mwa wiki kufanya majadiliano na maafisa jeshi wa Mali waliompindua Rais Ibrahim Boubacar Keita Agosti 18 ili kuurejesha utawala wa kiraia nchini humo. Hata hivyo siku tatu za mazungumzo hayo zimekwisha bila ya kufikiwa uamuzi kuhusu muundo wa serikali ya mpito.
Kiongozi aliyewaongoza wanajeshi katika mapinduzi huko Mali alisema baada ya kunyakua madaraka kwamba, wamechukua hatua hiyo kwa sababu nchi ilikuwa inatumbukia katika hali ya mchafukoge na ukosefu wa usalama ambavyo ni natija ya serikali dhaifu.
Ofisi ya Rais wa Nigeria ilisema kuwa, Goodluck Jonathan, Mpatanishi wa Jumuiya ya Ecowas alisema kuwa wafanya mapinduzi nchini Mali wanataka kuongoza kipindi cha mpito nchini humo kwa muda wa miaka mitatu kabla ya uchaguzi.
Hata hivyo mpatanishi huyo alisema kuwa, wamewaeleza wafanya mapinduzi hao wa Mali kwamba, jumuiya ya Ecowas itakubali serikali ya mpito chini ya uongozi wa kiraia au iongozwe na afisa jeshi mstaafu, ambayo itapasa idumu kwa muda wa miezi sita au tisa, na au kama ni zaidi, basi iweko madarakani kwa muda wa miezi 12.
Mazungumzo kati ya wawakilishi wa mataifa ya Afrika Magharibi na viongozi wa jeshi la Mali yameshindwa kufikia makubaliano ya jinsi ya kurejesha utawala wa kiraia nchini humo baada ya mapinduzi ya wiki iliyopita.
Mazungumzo nchini Mali yanayolenga kutatua mzozo wa kisiasa unaoendelea kufuatia mapinduzi yaliofanyika wiki iliopita yamemalizika bila makubaliano.
Viongozi wa mataifa ya magharibi mwa Afrika walisema kwamba rais aliyeondolewa madarakani, Ibrahim Keita , anafaa kurudishwa madarakani.
Lakini wajumbe hao kutoka kwa shirika la Ecowas walishindwa kuwaelewesha viongozi hao wa jeshi kwamba huo ndio uliokuwa uamuzi mzuri.
Keita alikabiliwa na maandamano makubwa kabla ya mapinduzi yake na raia wengi nchini Mali wameunga mkono kuondolewa kwake.
Msemaji wa jeshi, Kanali Ismael Wague alinukuliwa na Reuters akisema kwamba baada ya mazungumzo kuisha uamuzi wa mwisho kuhusu serikali ya mpito utatolewa na raia wa Mali wenyewe.
Lakini wazo la Keita kurudi madarakani huenda lilikataliwa na rais huyo mwenyewe, kulingana na chombo cha habari cha AFP.
Kilinukuu taarifa tofauti kutoka kwa pande hizo mbili zilizosema kwamba rais huyo amekuwa katika kizuizi tangu mapinduzi hayo Jumanne iliyopita na kwamba hangetaka kurudi madarakani
Kundi la wapatanishi linaloongozwa na aliyekuwa rais wa zamani wa Nigeria, Goodluck Jonathan litaripoti kwa viongozi wa serikali za Afrika kuhusu hatua zilizopigwa kulingana na kanali Wague alienukuliwa akisema.
Mazungumzo hayo yalianza kwa maelezo machache siku ya Jumamosi na kuendelea siku ya Jumapili na Jumatatu. Mwisho wa kikao bwana Jonathan alisema: “Tumeafikiana baadhi ya makubaliano lakini hatujapata mwafaka kuhusu masuala yote”.
Wiki iliyopita, maelfu ya raia waliandamana katika barabara za mji mkuu wa Bamako, ili kusherehekea mapinduzi hayo ambayo yalishutumiwa kote duniani.
AFP