30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Walimu wawili jela miaka 30 kwa kumbaka mwanafunzi

Na Nathaniel Limu-Iramba

WALIMU wawili wa Shule ya Sekondari Kata ya Kizaga, Wilaya ya Iramba mkoani Singida, wamehukumiwa kwenda jela miaka 30 kila mmoja, baada kukutwa na hatia ya kumbaka kwa zamu mwanafunzi wao mweye umri wa miaka 15 aliyekuwa akisoma kidato cha pili.

Waliohukumiwa ni Ernest Emmanuel (25) na Onesmo Bida (28), huku wenzao wawili ambao pia wanatuhumiwa kumbaka mwanafunzi huyo, kesi yao bado inaendelea.

Walimu hao wanne, wanadaiwa kumbaka mwanafunzi huyo kwa zamu huku wakijua kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria namba 130 kifungu (1) kifungu kidogo (2) (E) kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Lyoba Mkambala, alidai mahakamani hapo mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Iramba, Makwaya Charles, kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti toka Machi 2 mwaka jana hadi mwanzoni mwa mwaka huu.

Mkambala alidai mshtakiwa Ernest Emmanuel, alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na dada wa mwanafunzi huyo.

Alidai Machi 20 mwaka jana, saa 2 usiku, mwanafunzi huyo alienda nyumbani kwa shemeji yake Emmanuel kwa lengo la kuangalia sinema (movie).

“Baada ya kumaliza kuangalia ‘movie’, mwanafunzi huyo aliamua kurejea kwenye nyumba ambayo alikuwa amepanga. Mwalimu Emmanuel aliamua kumsindikiza na kuingia naye chumbani.

“Mwanafunzi alimbebeleza mwalimu wake ambaye pia ni shemeji yake arudi kwake ili yeye aweze kujisomea, lakini mwalimu alikataa na kisha kumshika kwa nguvu na kumwingilia kimwili,” alidai Mkambala.

Alidai kuwa Januari 21, mwaka huu, wazazi wa mwanafunzi huyo walimchukua binti yao na kwenda naye hadi kwa mkuu wa shule kushtaki kwamba mtoto wao anakataa shule.

“Mwanafunzi huyo baada ya kuhojiwa, alisema ana mimba. Pia alitumia nafasi hiyo kutaja walimu waliomwingilia kimwili kuwa ni Ernest Emmanuel, Onesmo Bida, Keneth Komba na Ally Pangu, aliosema kila mmoja alimbaka kwa muda wake,” alidai.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mkambala aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa washtakiwa na iogopeshe walimu wengine wanaotarajiwa kubaka wanafunzi.

Washtakiwa kila mmoja kwa wakati wake, alitoa maombolezo yanayofanana kwamba bado ni vijana wadogo na wanategemewa kwa kiwango kikubwa na familia zao, hivyo wapewe adhabu nafuu.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Makwaya, alisema kitendo walichofanya walimu hao ambao wamepwa jukumu la kuwatunza na kuwalinda wanafunzi waweze kufikia malengo yao hakivumiliki.

“Wazazi wa mwanafunzi huyu, waliwekeza kumwendeleza mtoto amalize masomo yake na kuwa na elimu ambayo ingesaidia wazazi hao kumaliza safari yao hapa dunia vizuri.

“Lakini ndoto hiyo imepotezwa na walimu. Kwa kosa lenu la ubakaji nafungwa mikono kulegeza hukumu, hivyo mtaenda jela kila mmoja miaka 30,” alisema hakimu huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles