NA RAMADHAN HASSAN, DODOMA
SERIKALI imesema itachukua hatua stahiki za sheria kwa walimu wa Shule ya Sekondari ya Mbeya waliompiga na kumjeruhi mwanafunzi ushahidi utakapokamilika.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuphu Masauni, alipojibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema).
Mbunge alitaka kujua, kauli ya serikali ya kuondoa sintofahamu ya kuachiwa huru bila kuchukuliwa hatua za sheria walimu wa shule ya sekondari Mbeya waliompiga na kumjeruhi mwanafunzi.
“Hivi sasa kuna sintofahamu kubwa kwa wananchi na hasa wazazi wa mwanafunzi aliyepigwa na kujeruhiwa, baada ya walimu hao kuachiwa huru.
“Sasa nataka kujua ni nani aliyeruhusu kuachiwa huru kwa walimu hao?”alihoji Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu.
Akijibu, Masauni alisema suala hilo ni mtambuka na linashughulikiwa na taasisi zaidi ya moja.
Alisema kwa upande wao polisi kupitia Mwendesha Mastaka Mkuu wa Serikali (DPP), anaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo na mara tu utakapokamilika hatua za sheria zitachukuliwa dhidi ya walimu hao.