Na Norah Damian, Mtanzania Digital
Walimu wa shule mbalimbali za sekondari katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wamepatiwa mafunzo kuhusu mtaala wa ujenzi wa umahiri (Competence Based Curriculum) ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji unaolenga kumjengea mwanafunzi mwelekeo wa kutenda.
Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Halmashauri hiyo huku wawezeshaji wakiwa ni Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), yameshirikisha walimu kutoka Shule za Sekondari Zanaki, Mnazi Mmoja, Magoza, Kimanga, Mzizima na Alrahma.
Akizungumza Machi 3, 2023 wakati wa mafunzo hayo, Mkuza Mitaala kutoka TET, Sophia Amasi, amesema mtaala huo unaweka mkazo kwenye ufundishaji na ujifunzaji unaozingatia ujenzi wa umahiri.
“Huu ni mfumo mpya wa ufundishaji unaendelea kutumika, baada ya mafunzo haya tunatarajia walimu wapate mbinu stahiki, kuinua viwango vyao vya utendaji kazi na kuongeza ufaulu wa wanafunzi,” amesema Amasi.
Amesema kupitia mafunzo hayo walimu wanafundishwa mbinu za ufundishaji na ujifunzaji namna ya kutunga maswali ya ujenzi wa umahiri na kufanya tathmini inayozingatia ujenzi wa umahiri.
Amesema malengo ya TET ni kuhakikisha walimu wote nchini wanafikiwa na kwamba tayari wametoa mafunzo hayo katika Wilaya za Mbarali, Kibiti na Kisarawe.
Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Zanaki, Delvine Koka, ameishukuru halmashauri kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yatawawezesha walimu kuweza kuufahamu mtaala huo.
“Huu ni mtaala mpya na walimu wengi hawana ufahamu mzuri hivyo, ni vema walimu tukapata mafunzo,” amesema Koka.
Mmoja wa washiriki Mwalimu Nchwembu Fabian wa Shule ya Sekondari Zanaki, amesema ameshauri mafunzo yawe endelevu kwani yanawawezesha walimu kujua mbinu tofauti za ufundishaji na utungaji maswali ya mitihani.
“Mtaala huu unaleta ushindani kwa wanafunzi, wanaweza kuwa kwenye makundi wanajadili halafu mwalimu unasikiliza wanafunzi wameelewa nini, mwalimu ana – ‘share’ mawazo na kila mwanafunzi anafanya kile alichokielewa,” amesema Mwalimu Fabian.
Mshiriki mwingine Mwalimu Kudra Hashimu wa Shule ya Sekondari Mnazi Mmoja, amesema mfumo wa awali wanafunzi wengi walikuwa wakikariri lakini kupitia ujenzi wa umahiri utapima vizuri uelewa wa wanafunzi.