Na SAMWEL MWANGA
WALIMU katika Wilaya ya Maswa wametakiwa kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi hususan kipindi hiki ambacho taifa linaelekea kwenye uchumi wa viwanda kuweza kupata wataalamu wa kutosha.
Pia waratibu elimu kata na walimu wakuu wametakiwa kusimamia kwa ukamilifu masuala yote ya taaluma katika shule za maeneo yao kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi.
Ofisa Elimu Msingi Wilaya ya Maswa, Simon Bujimu alikuwa akitangaza matokeo ya mtihani wa ujirani mwema wa darasa la saba wa wilaya za Maswa na Kwimba.
Alisema umefika wakati wa walimu wa shule za msingi wilayani humo kuwa wabunifu na kuwahamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.
Bujimu alisema masomo hayo ni chachu ya maendeleo ya nchi hasa katika kuelekea Tanzania ya uchumi wa viwanda.
“Wakati umefika kwa walimu wa shule za msingi kuongeza ubunifu tuweze kuwahamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.
“Masomo haya ni chachu ya maendeleo nchini hasa tunapoelekea katika Tanzania ya uchumi wa viwanda,”alisema.
Alisema serikali inatambua walimu ni injini ya elimu kwa sababu bila wao elimu haiwezi kusonga mbele hivyo wanapaswa watumie nafasi zao kuhakikisha serikali inapata wataalamu waliobobea katika masomo ya sayansi kwa kuwajengea misingi bora.
“Hatuwezi kupata wataalamu wa kutosha viwandani kama hatutahamasisha masomo ya sayansi shuleni…. itakuwa na utegemezi mkubwa kuwa na wataalamu kutoka nje ya nchi jambo ambalo si zuri,”alisema.
Alisema shule 10 zilizofanya vizuri katika ufaulu wa jumla wilayani humo zitapongezwa na nyingine 10 zilizofanya vibaya zitasaidiwa kuona ni wapi zimeshindwa ili nazo ziweze kufanya vizuri.
Bujimu alizitaja shule 10 zilizofanya vizuri katika wilaya hiyo kwa ufaulu wa jumla kuwa ni shule za msingi Mwatumbe, Mwanhengele, Mwaliga, Mwandu, Mwabomba, Mwanganda, Shishiyu, Kadoto, Igwata na Mlimani.
Shule nyingine 10 zilizofanya vibaya kwa ufaulu wa jumla ni Ngongwa, Nguliguli, Mwamitumai, Malita, Kiloleli, Bushitala, Mpindo, Ikungulyankoma, Mwamanenge B na Iwelimo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Maswa, Dk. Fredrick Sagamiko alisema mitihani hiyo ya ujirani mwema ni mpango wa Mkoa wa Simiyu wa kujipima kitaaluma kwa wanafunzi wanaotegemea kufanya mitihani yao ya mwisho na wao wanatekeleza kwa vitendo.