Na BENJAMIN MASESE,MWANZA
NISEME hii ni aibu kwa Mkoa wa Mwanaza na watawala wake. Nimetangulia kusema hivyo kwa sababu Mwenge wa Uhuru umepiga hodi mkoani hapa tangu Agosti 26, mwaka huu na baadhi ya miradi imezinduliwa huku mingine ikikataliwa na kiongozi wa Mwenge kitaifa, Charls Kabeho.
Lakini wakati Mwenge huo ukiendelea kutembelea wilaya mbalimbali na kuzindua miradi ya maendeleo, binafsi nimeshangazwa na kitendo cha miradi mingi ya jiji la Mwanza kuwa na kasoro na kukataliwa kuzinduliwa.
Ipo baadhi ya miradi ambayo ilikuwa ikitarajiwa kuzinduliwa ndani ya Wilaya ya Nyamagana lakini Mwenge haukufika kwa kile kilichoelezwa kwamba bado haijakamilika ilihali kulikuwa na maandalizi yote ya kuzinduliwa.
Tukumbuke tayari barabara zimelimwa kwenda kwenye miradi hiyo na kuna gharama tayari zimetumika lakini kwa kuwa viongozi walijua ama wamezoea kudanganya, mwaka huu wameumbuka baada ya kutambua kwamba Charles Kabeho ambaye inadaiwa ni mhandisi hataki mchezo.
Miradi iliyokuwa izinduliwe katika Kata ya Kishili jijini Mwanza imeondolewa kwa kile kilichodaiwa kuna mapungufu.
Tunashukuru kwa mamlaka ya uteuzi wa kiongozi wa Mwenge kitaifa, Kabeho kwani ameonekana kuwa tofauti na watangulizi wake ambao hata walipopewa taarifa za udanyanyifu wa miradi kadhaa walikuwa hawachukui hatua kama ilivyo sasa.
Ipo baadhi ya miradi ambayo mwaka jana ilizinduliwa mkoani Mwanza licha ya wasamaria wema na wananchi kuipinga mbele ya kiongozi wa Mwenge, lakini ikazinduliwa ambapo leo hii baadhi haifanyi kazi ama hayajatekelezwa yale maagizo yaliyotolewa.
Unaweza kujiuliza maswali mengi juu ya taarifa za Mwenge kwenye vyombo vya habari zinavyoripotiwa, baadhi ya mikoa zinatangazwa sana na vyombo mbalimbali kila wilaya na kinachofanyika lakini mikoa mingine unaweza usijue kama kuna mbio hizo.
Kwa upande wa mikoa ambayo taarifa zinatolewa sana ni dhahiri wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi na waratibu wa Mwenge wamejipanga na kushirikiana na waandishi wa habari kwa ukaribu wakitambua wazi umuhimu wa tasnia hiyo kuwafikishia wananchi taarifa kupitia vyombo vyao.
Kwa bahati mbaya, ile mikoa ambayo unasikia ukimya na hakuna taarifa za Mwenge kwamba hakuna ushirikiano kati ya waandishi na viongozi waliopewa dhamana ama kwa makusudi, watawala hao wanajua wazi miradi hiyo ina kasoro hivyo kuwashirikisha waandishi wa habari wanaweza kuwaharibia.
Inasikitisha sana kuona kiongozi wa mkoa anashindwa kufanya mkutano kwa waandishi wote kuwajulisha ujio wa mwenge na kuainisha miradi itakayozinduliwa ama kukaguliwa badala yake wanabagua vyombo vya habari huku wakijionesha wazi kufanya kazi na tovuti za watu binafsi, blog, baadhi ya televisheni na mitandao ya kijamii.
Unaweza kushangaa ukiwa kwenye chombo cha usafiri unakutana na askari polisi wa barabarani akiwasimamisha na kuwataka kuegesha gari pembeni, unapomwuliza anakwambia Mwenge wa uhuru unapita, ni jambo la kushangaza.
Hili linadhihirisha kuwa wapo viongozi waliopewa dhamana na Rais Dk. John Magufuli kumsaidia kuwaongoza wananchi ngazi ya mkoa, wilaya na halmashauri lakini binafsi nasema kiatu walichovalishwa kimepwaya.
Rais Magufuli anapaswa kutambua ipo baadhi ya mikoa na wilaya zake imedumaa kifikra katika kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama chama kilichopewa ridhaa na wananchi kuwaongoza, wapo viongozi ambao ikitokea wakahamishwa ama kuondolewa wadhifa wao hakuna alama yoyote wanayoiacha inayoonyesha mchango wake.
Sote tunatambua moja ya kero kubwa kwa wananchi ni migogoro ya ardhi lakini ipo baadhi ya mikoa na wilaya watawala wake hawana mchango.
Viongozi wa mikoa na wilaya wamebaki kusubiria kutekeleza maagizo ya waziri, waziri mkuu ama Rais Magufuli, hao ndiyo binafsi nasema viatu walivyovalishwa vimepwaya kwa sababu wamekosa ubunifu wa kiutawala.
Ni juzi tu Rais Magufuli amekutana na malalamiko Sengerema juu ya wamachinga kunyanyaswa ambapo alitoa maelekezo ambapo tayari uongozi wa wilaya hiyo umewalipa machinga Sh 5,780,000 kama fidia ya kuchukuliwa mananasi yao.
Wakati wanatoa fedha hizo kwa machinga, ndani ya wilaya hiyo kuna shule ya sekondari wanafunzi wa kidato cha kwanza hawana darasa wala madawati wanakaa chini wakati wa masomo ambapo kilio hicho kimefikishwa kwa Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Sasa unaweza kujiuliza ina maana hakuna kiongozi aliyewaza juu ya hilo badala yake wakaelekeza nguvu zao kwa wamachinga, umefika wakati wa kubadilika.
Binafsi naomba nimalize kwa kuwaomba mlioaminiwa na Rais Magufuli ongezeni jitihada za kumsaidia katika maeneo yenu, acheni ubaguzi, fitina, ridhikeni na mnachopata, waacheni kuwasumbua wafanyabiashara, nendeni kwa wananchi wana kero nyingi, wasimamieni ipasavyo watumishi walio chini yenu.