WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), , amewataka wakurugenzi wapya a kuacha kufanya kazi na mitandao ya jamii kwa vile imekuwa ikitoa habari ambazo si sahihi.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini hapa alipozungumza na wakurugenzi hao baada ya kuapishwa.
Alisema ni lazima wafanye kazi kwa kufuata kanuni na taratibu na siyo kila wanachokiona kukiweka katika mitandao ya jamii.
“Msifanye kazi na mitandao ya jamii kwa sababu mingi ni ya uzushi na imekuwa ikidanganya watu, siyo kila unachokiona unakiweka katika mtandao,’’alisema.
Simbachawene alitoa mfano wa taarifa iliyotolewa katika mitandao ya jamii hivi karibuni kuwa Ofisi ya Rais Tamisemi imeanza kuwaruhusu waombaji wa ajira za ualimu kuanza kutumia mfumo wa maombi ya ajira za ualimu(On line Teachers Employment Application System-OTEAS) kuwa siyo za kweli.
“Imetuletea shida kubwa, inawaumiz,a unakuta mtu ametoka kijijini ametumia zaidi ya Sh 100,000 kuja mjini kutuma maombi hayo halafu anakuta siyo ukweli hii mitandao tuachane nayo,’’alisema.
Aliwataka wakurugenzi hao kutokaa ofisini na badala yake waende kusikiliza kero za wananchi kwenye maeneo yao.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mejenimenti ya Utumishi ya Umma, Angella Kairuki, aliwataka wakurugenzi hao kufuatililia na kutoa mrejesho wa matamko yanayotolewa na viongozi wakuu wa nchi, kuzingatia kanuni na taratibu katika utendaji wao wa kazi na kufuatilia fedha za miradi zanazoletwa katika halmashauri zao.
“Nawaomba mjitahidi muwe makini katika utendaji kazi wenu hakuna hata mmoja aliyepata ukurugenzi kwa bahati mbaya.
“Mwende mkasimamie maadili pia mjue fedha za kila mradi gharama yake ni shilingi ngapi… nawaomba mkasimamie maofisa utumishi kwa sababu wapo ambao wamewapitisha watumishi hewa,” alisem Kairuki.
Wakurugenzi walioapishwa na Halmashauri zao katika mabano ni Mwantumu Dau (Bukoba), Frank Bahati (Ukerewe), Hudson Kamoga (Mbulu), Mwailwa Pangani (Nsimbo), Godfrey Sanga (Mkalama) na Yusuph Semuguruka(Ulanga).
Wengine ni Bakari Mohammed (Nachingwea), Juma Mnweke (Kibondo), Batamo Ndalahwa (Moshi), Waziri Mourice (Karatu), Fatma Latu (Bagamoyo), Godwin Kunambi (Manispaa Dodoma) na Elias Ntiruhungwa (Tarime Mjini).