Na AMINA OMARI
PAMOJA na kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa, wakulima wengi bado wamekuwa wakitumia mbinu duni za uhifadhi wa mazao yao.
Mbinu hizo ni pamoja na maghala ya kienyeji ambayo huyaweka mazao katika hatari mbalimbali ikiwamo kushambuliwa na wadudu waharibifu.
Upotevu wa mazao unaendelea kuwa moja ya changamoto kubwa zinazowakabili wakulima. Mazao mengi yamekuwa yakipotea kuanzia katika kipindi cha uvunaji mashambani, usafirishaji, uanikaji hadi katika hatua ya mwisho ya uhifadhi.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 20 hadi 40 za mazao yanayovunwa na wakulima hasa mahindi, hupotea kutokana na mbinu duni ambazo hufanya mazao kushambuliwa na wadudu waharibifu.
Wakulima wengi wamekuwa wakitumia dawa za viwandani kwa ajili ya kunyunyuzia mazao hayo ili yasiweze kuharibika bila kujua baadhi ya kemikali zina madhara makubwa kwa afya ya binadamu wanaotumia vyakula hivyo.
Kutokana na changamoto hiyo, ndipo Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA) kupitia mradi wake wa African Rising wamekuja na suluhisho la kumsaidia mbinu mkulima ya kuhifadhi mazao yake.
Mradi huo umeweza kuja na teknolojia ya kubuni mifuko ya kinga ya njaa maarufu mifuko ya PICS ambayo ni maalumu kwa ajili ya kuhifadhia mazao bila ya kutumia kemikali.
Kwa hapa nchini, mifuko hiyo inazalishwa na kiwanda cha kuzalisha vifungashio na mifuko ya plastiki cha PPTL kilichoko jijini Tanga.
Suraj Devan ni Mkurugenzi wa kiwanda hicho, anasema mifuko hiyo imekuja kuwa mkombozi wa mkulima kwani hawatalazimika kutumia kemikali tena kwa ajili ya kuhifadhi mazao yake.
“Mifuko hii imekujaa maalumu kwa ajili ya kuachana na matumizi ya kuhifadhi mazao kwa njia ya kemikali kwa kuwa sasa mkulima ataweza kuhifadhi mazao yake katika mfuko maalumu ambao haupitishi hewa na kuruhusu mdudu wa aina yoyote kupenya,” anasema Devan.
Anasema mfuko huo umetengenezwa kwa mifuko aina mbili ambapo kwa ndani kuna mfuko wa plastiki ambao haupitishi hewa na nje umezungushiwa mfuko wa safleti.
Devani anaendelea kufafanua kuwa, uhifadhi huo unamsaidia mkulima mdogo kupata uhakika wa mazao yake kama alivyoyavuna shambani bila ya kuathiriwa na wadudu.
“Katika msimu huu wa mvua chache, mifuko hiyo itasaidia kuwa mkombozi mkubwa wa wakulima kwani licha ya kupata mazao kidogo, lakini hatalazimika kununua dawa kwa ajili ya kupulizia mazao hayo,” alibainisha Mkurugenzi huyo.
Hata hivyo, licha ya mifuko hiyo kuzalisha hapa nchi lakini bado mwitiko wa matumizi yake ni mdogo tofauti na nchi za nje ambako kuna uhitaji mkubwa sana wa mifuko hiyo.
Anasema kwa upande wa Mkoa wa Tanga, ni wilaya tatu pekee ambazo wakulima wake wameweza kuona manufaa ya kutumia mifuko hiyo kwa ajili ya kuhifadhia mazao yao.
“Wilaya za Muheza, Pangani na Muheza pekee ndio wakulima wake wamepata mwamko wa kutumia mifuko hiyo baada ya kuona faida yake. Wameweza kuhifadhi mazao kwa zaidi ya miaka mitatu bila ya kuharibika,” anasema mkurugenzi huyo.
“Soko letu kubwa lipo katika nchi za Kenya, Burundi, Rwanda na Somalia ambako kwa mwaka jana pekee tuliweza kuuza mifuko laki nne na mwaka huu matarajio yetu ni kuuza hadi mifuko laki sita,” anasema.
Anafafanua kuwa, kwa hapa nchini matumizi ya mifuko hiyo yameweza kuwafikia wakulima takribani 3600 katika maeneo mbalimbali nchini kote na kuongeza kuwa kampuni yake inaendelea kuwahamasisha wengine zaidi ili waweze kutumia mifuko hiyo.
Kwa upande wake Meneja Uzalishaji wa mifuko hiyo, Ladislaus Ngingo, anaeleza kuwa walianza kuzalisha mifuko hiyo mwaka 2014 na kuweza kuisambaza katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Aidha, ameongeza kuwa mifuko hiyo ina uwezo wa kuhifadhi mazao kwa kipindi cha miaka miwili bila kuharibiwa na wala kuathiriwa na wadudu.
“Mifuko ya PICS imekuja kwa ajili ya kubadilisha jamii kuachana na matumizi ya kemikali katika mazao ambayo wakati mwingine kemikali hizo zimekuwa zikileta athari kwa walaji,” anasema meneja huyo.
Kwa Mkoa wa Tanga, mifuko hiyo imeweza kusambazwa kwa wilaya za Pangani, Lushoto, Korogwe na Kilindi ambazo ndiyo wilaya zinazoongoza kwa kilimo cha mahindi.
Hata hivyo, Ngingo anasema changamoto kubwa ni wasambazaji wa pembejeo ambao ndio wauzaji wakuu wa mifuko hiyo kukosa mitaji ya kununua kwa wingi bidhaa hiyo kwa ajili ya kuwauzia wakulima.
Licha ya mwitiko mkubwa wa wakulima kutumia bidhaa hiyo, anasema wamekuwa wakikwamishwa na wasambazaji hao ambao hawana fedha za kutosha kununua mifuko hiyo na kuwauzia wakulima.
“Kutokana na umuhimu wa mifuko hiyo, ningeziomba halmashauri kuingia mikataba na kiwanda na kununua mifuko hiyo kwa ajili ya wakulima walioko katika maeneo yao na kuwasaidia kusambaza mifuko hiyo katika maeneo mbalimbali hususani vijijini ambako ndiko kuna wakulima wengi,” anashauri Meneja huyo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella, amewaagiza maofisa ugani mkoani hapa kutoa elimu kwa wakulima juu ya namna bora ya kuhifadhi mazao yao kwa kutumia mifuko ya PICS ambayo uhifadhi wake hauhitaji
kunyunyuzia madawa yenye kemikali.
Anasema iwapo wakulima wataweza kuelekezwa manufaa ya kutumia mifuko hiyo kwa ajili ya kuhifadhia mazao yao, wataweza kuepukana na kutumia njia ya kienyeji za kutumia maghala ambayo wakati mwingine wanapata hasara ya mazao yao kuharibika.
“Wakulima wetu hawana uelewa wa kutosha kutumia mifuko hii, hivyo ni wajibu wa maofisa ugani kuwapa elimu ambayo itawasaidia kuachana na jia za kuhifadhi kizamani ambazo zimekuwa zikiwasababishia hasara ya mazao yao kwa kuharibiwa na wadudu,” anaeleza Shigella.
Anaendelea kueleza kuwa, kutokana na maendeleo ya kiteknolojia yaliyopo kwa sasa, watu wengi wanajiepusha na matumizi ya vyakula au bidhaa ambazo zimehifadhiwa kwa kutumia madawa.
Baadhi ya wakulima wilayani Muheza wanaotumia mifuko hiyo, walisema kabla ya kutumia teknolojia hiyo walikuwa wakipoteza kiasi kikubwa cha mazao yao kutokana na kuhifadhi kwa njia za kienyeji.
Andrew Samweli anasema baada ya kupatiwa elimu juu ya kutumia mifuko hiyo, wakulima waliamua kuhifadhi mahindi yao vizuri na baada ya miezi sita yalikuwa katika hali nzuri tofauti na yale yaliyohifadhiwa kwa kutumia kemikali za viwandani.
“Kwa kweli njia ya kuhifadhi mazao kutumia mifuko ya PICS imekuwa msaada mkubwa kwetu kuanzia katika familia hadi katika masoko kwani yameweza kuuzika kirahisi tofauti na yale yaliyokuwa na madawa,” anaeleza.
Naye Hellen Mhando anasema kuwa mifuko hiyo inasaidia kuhifadhi chakula na kuepukana na njaa katika kaya kwani awali mahindi yalikuwa yakiharibika sana.
“Unaweza kuvuna debe saba za mahindi lakini kutokana na uhifadhi duni wakati wa kuyauza au matumizi mengine, unakuta umebakiwa na debe tano; debe mbili zote zimeharibiwa kwa kuliwa na wadudu,” anasema.