yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi, ambayo kwa kiasi kikubwa yakekuwa yakisababisha minazi mingi kufa na hivyo zao hilo kuanza kuadimika katika baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakilima kwa wingi zao hilo.
Kwa Mkoa wa Tanga, zao hilo linazalishwa kwa wingi wilayani Pangani, ambapo wakazi wake waliokuwa wakiishi kwa kutegemea nazi huenda wakakumbwa na hali mbaya ya maisha ikiwamo njaa kutokana na zao hilo kuyumba wilayani humo.
Kuyumba kwa zao hilo kunasababishwa na kuibuka kwa magonjwa huku mingine ikiwa imezeeka.
Kufuatia hali hiyo, Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM), Jumaa Aweso, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, anawaomba watalaamu wafanye utafiti utakaofikia mwisho wenye manufaa ili kuweza kuokoa jamii ya maeneo ya pwani hususani wilayani humo ili waweze kurudisha uchumi wao unaotokana na nazi.
Anasema magonjwa yanayoshambulia nazi bado yanaendelea kuwatesa wakazi wa wilaya hiyo na hivyo hawajui wafanye nini, ili kuweza kukabiliana nayo huku minazi ikiendelea kuathirika kwa asilimia kubwa na kusababisha wakulima kukata tamaa juu ya hatma yao.
Aweso anataja miongoni mwa magonjwa hayo kuwa ni mnyauko, ambao husababisha minazi kunyauka na kuanza kupukutika.
Anasema ni miaka 30 sasa tangu ugonjwa huo uingie wilayani Pangani na kuvamia minazi, hali inayosababisha minazi mingi kufa, na kwamba hali hiyo inaweza kuendelea iwapo hatua madhubuti ya kulinusuru hazitachukuliwa.
“Ugonjwa huu wa minazi hapa Pangani umekuwa hatari kama ilivyokuwa Ukimwi kwa binadamu hivyo, niwaombe watalamu waweze kufanya utafiti wenye manufaa kwani nazi zimekuwa na shughuli nyingi ukiacha kupikia, machicha yake unaweza kusingwa na kuwa na ngozi nyororo,” anasema.
“Lakini pia mbata na muhogo shughuli zake ni nzito, inaleta heshima kwenye ndoa hivyo ndugu zetu wataalamu tusaidieni zao hili ni muhimu kwa Wilaya ya Pangani, linasaidia kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja mmoja, wilaya na mkoa kwa ujumla,” anasema.
Kwa kuonyesha kuunga mkono suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainabu Abdallah, anasema zao hilo limekumbwa na ugonjwa uliosababisha uzalishaji kushuka kutoka hekta 11,000 hadi hekta 6,595.
Anasema ugonjwa wa nyongea, ukame na mengine ikiwamo kuchanwa mbao kwa ajili ya ujenzi imekuwa ni kikwazo kikubwa kwa wakulima.
Anasema minazi inalimwa na wakulima wadogo na wakubwa, ambapo wakulima wadogo wana wastani wa ekari tano hadi 10 na wakubwa wanamiliki wastani wa ekari 50 hadi 200; ambao wanafikia takribani watu 15.
Anaeleza kwamba minazi mingi kwa sasa inapatikana bonde la Mauya pembezoni mwa Mto Pangani, Kata ya Ubanga, Masaika na Bushiri.
Kutokana na uwapo wa changamoto hiyo, Mkuu huyo wa wilaya anamuomba Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba, kusaidia kupatikana kwa ufumbuzi wa magonjwa hayo yanayosumbua minazi na kusababisha uzalishaji kushuka kwa kasi.
Anasema vipo viwanda ambavyo vinategemea zao hilo kuleta maendeleo ya uchumi wilayani huku akieleza watakapopata ufumbuzi uzalishaji utaongezeka.
“Lakini pia, tunakuomba Naibu Waziri, tuna upungufu mkubwa wa maafisa ugani katika baadhi ya maeneo hivyo, tunakuomba ulishughulikie suala hilo ili liweze kuwa na tija kwa wakulima wetu wilayani Pangani,” anasema.
Naye Ofisa Tawala wa Wilaya ya Pangani, Gibson George, anasema watafiti ambao wanazungumzwa hawajawahi kufika wilayani humo lakini alisikia kwa wazee wake kwamba huko nyuma ilitengwa bajeti takribani Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya kazi hizo na nyengine zimekwisha tumika.
Anasema hata hivyo, bado hawajafika wilayani humo na kama wangefika, wangepata majibu ambayo yangesaidia kupunguza tatizo, kwani ni muda mrefu sasa wakulima wanahangaika kutafuta dawa bila mafanikio.
“Ili kuendeleza kilimo, ni lazima kuwekeza nguvu katika kufanya tafiti kwa sababu huko ndiko kunaweza kupatikana majibu sahihi yanayoweza kumkomboa mkulima nchini,” anasema.
Akizungumzia zao hilo, Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba, anasema zao la minazi lina changamoto kubwa kwa zaidi ya miaka 30 sasa.
Anasema siku zote hizo wakulima wanatafuta suluhu bila mafanikio, huku akieleza kwamba changamoto kubwa inayokwamisha zao hilo ni mabadiliko ya tabianchi.
Anasema tatizo jingine ni ujio wa mbegu za kisasa ambazo haziendani na hali ya nchi hivyo, sasa hivi kinachotakiwa kufanywa ni kuimarisha vituo vya utafiti, hasa cha utafiti wa minazi kilichopo Mikocheni.
Anasema kuna haja ya kurudi kwenye kuzalisha miche kwa kutumia minazi ya asili inayokabiliana na hali ya hewa na ikolojia ya nchi yetu.
Naibu Waziri huyo anasema kuwa sasa hivi wameanza kitalu cha kuzalisha miche pale Bagamoyo, ambayo itasambazwa nchi nzima ili kuimarisha kilimo cha nazi.
Aidha, anasema kuwa zao hilo limeendelea kushuka bei kutokana na ushindani mkubwa uliopo katika soko la ndani, soko la kanda na kimataifa kutokana na uwapo wa bidhaa mbadala.
“Bei ya nazi inapopanda, watu wanakimbilia kwenye mafuta, vitu vya kuchemsha, na kila tunapotumia mafuta mahitaji yanapungua hatimaye nazi zinakosa soko,” anasema Naibu Waziri huyo.
Anaeleza mkakati uliopo sasa ni kuhakikisha kunakuwapo viwanda vitakavyoongeza thamani ya bidhaa zinazotokana na nazi nchini.
Nchi zinazoongoza kwa uzalishaji
Indonesia ndio nchi inayotajwa kuongoza kwa uzalishaji wa nazi duniani, ikiwa inazalisha asilimia 35.8 ya mbata. Kwa mwaka 2015 nchi hiyo ilizalisha tani milioni 19.5 ikifuatiwa na Philippines ambayo ilizalisha tani milioni 18.3.
India ambayo pamoja na Indonesia zinatajwa kuwa ni asili ya minazi, mwaka 2015 ilishika nafasi ya tatu kwa kuzalisha tani milioni 11.93 za mbata huku Brazil ikiwa ya nne kwa kuzalisha tani 2,820,468. Katika orodha ya nchi 10 vinara wa uzalishaji wa mbata duniani, Sri Lanka ilishika nafasi ya tano kwa kuzalisha tani milioni 2.2; Vietnam nafasi ya sita kwa kuzalisha tani 1,312,200; Papua New Guinea ilizalisha tani milioni 1.2; Mexico tani milioni 1.1; Thailand tani milioni 1.01 na Malaysia ilizalisha tani 605,000.
Nazi zina soko kubwa duniani kwa sababu mbata inauzwa viwandani kwa ajili ya kutengeneza mafuta.
Kwa upande wa Bara la Afrika, Tanzania inaongoza kwa uzalishaji wa zao hilo ambapo hulima hekta 350,000.
Kwa Tanzania, inaelezwa kuwa Waarabu ndiyo waliosambaza zao hilo katika maeneo mbalimbali nchini, hasa ukanda wa pwani kama vile Tanga, Bagamoyo, Unguja na Pemba kwa kutaja baadhi.
Tangu awali, zao hilo limekuwa tegemeo la kiuchumi kwa wananchi wa Mafia, ambapo ukiacha mashamba rasmi, kila nyumba ina wastani wa minazi miwili au mitatu.