30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

WAKULIMA WA CHAI NJOMBE KUNOLEWA NI JAMBO JEMA

Na MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya Kuhudumia Wakulima Wadogo Njombe (Njombe Outgrowers Service Company- (NOSC), imejikita katika kuwafundisha wakulima wa chai kwa vitendo mkoani Njombe, ili kukuza tija katika kilimo cha chai, kuziba pengo la uhaba wa maofisa ugani na Tanzania kunufaika na bei nzuri ya chai ulimwenguni iliyopo sasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa NOSC, Filbert Kavia, ameeleza kwamba, kampuni hiyo imeanzisha utaratibu huu ili chai inayozalishwa na wakulima iwe ni ya daraja la juu, pato la wakulima liongezeke sana na Tanzania iingize fedha ya kigeni. Utaratibu wa aina hii unatumika nchini Kenya pia.

“Tumeanza na vikundi vinane ili kuona mwitikio wa wakulima na kupata uzoefu. Tutaongeza idadi ya vikundi mwakani. Utaratibu huu ni mzuri, kwa sababu unampa fursa mkulima kujifunza kwa vitendo. Kwa kawaida wakulima huelewa zaidi kwa kuona vitendo shambani.

“Vilevile nchi yetu ina uhaba wa maofisa ugani. Tunakusudia kutumia wakulima kuwafundisha na wakulima wenzao. Kama eneo linahitaji maofisa ugani 20, kwa utaratibu huu wanaweza kutumika chini ya hapo. Tunaamini kwa sasa tutapata mavuno mengi ya chai na yenye ubora  baada ya mafunzo haya,” amesema Kavia.

Akizungumza katika mahafali ya mwaka mmoja ya mafunzo ya kilimo kwa wakulima 206 hivi karibuni, Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji, Mkoa wa Njombe, Lameck Noah, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Christopher Ole Sendeka, amesema mkoa utapata fedha nyingi za kigeni kwa sababu zao la chai lina bei nzuri katika soko la kimataifa.

“Katika mkoa wetu tulijiwekea utaratibu kuwa kila mkulima alime mazao ya aina mbili, ya chakula na biashara. Kwa upande wa chai, tatizo lilikuwa ni aina ya miche, ilikuwa inachukua muda mrefu kukua, lakini tunaishukuru NOSC, imetuletea miche inayokua kwa miezi 12 mkulima anaanza kupata majani mabichi ya chai,” anasema Noah.

Alibainisha kuwa, elimu hiyo ina maana kubwa kwa mkoa wake, kwa sababu itawasaidia kulima kisasa na kuwaongezea kipato wananchi wa mkoa huo, lakini pia viwanda vitapata malighafi hiyo muhimu kwa ajili ya soko la ndani na nje.

“Tunafahamu chai inapendwa na mataifa ya Magharibi. Zao hili lina fedha nyingi za kigeni. Soko la chai lipo na tunawahakikishia wakulima serikali inahangaika kupata mnada wa chai katika ukanda huu badala ya kufanyika Mombasa, nchini Kenya.

“Elimu kwa wakulima kupitia huu mfumo ni suala zuri, kwa kuwa wakulima watakuwa na kilimo endelevu, waliofundishwa watawafundisha wenzao ili kupata mavuno mazuri na mazao yenye ubora. Tunafahamu katika eneo hili kuna kiwanda cha Uniliver kinakaribia kukamilika. Maana yake watahitaji majani mengi ya chai ili kulisha kiwanda. Wakiendelea kulima zaidi tutawavuta wawekezaji wengi zaidi katika mkoa wetu ili kufikia azama ya nchi ya viwanda,” anasema Noah.

Maelezo hayo yanadhihirisha namna NOSC walivyokuwa karibu na serikali, hasa viongozi wa serikali za mitaa, ambao ndio watendaji na ndio wanaokutana na wakulima wadogo kila siku.

Changamoto katika kilimo kwa sasa si pembejeo tena, changamoto kubwa ni elimu ya kilimo ambayo kutolewa kwake lazima kumnufaishe mkulima. Kilimo cha kibiashara ndicho kilichowaondoa wananchi wengi kwenye umasikini katika mataifa yaliyoendelea.

Sababu zipo mbili: Moja ni namna mkulima anavyolima kwa kufuata ushauri wa kitaalamu, lakini pia anajua ardhi gani inafaa kwa kilimo gani. Uzuri wa mkulima kupata elimu ni namna anavyotambua kukabiliana na masoko, hivyo hata namna ya kuuza mazao baada ya kuvuna inakuwa rahisi.

Pili mkulima anapata fursa ya kushauriana na wenzake aliopata nao mafunzo, tazama wakulima wadogo zaidi ya 200 wanapopata mafunzo kwa pamoja maana yake kila mkulima akisambaza mafunzo hayo kwa wanakijiji wawili, ndani ya muda mfupi wakulima zaidi ya 100 watakuwa na elimu ya kutosha kuhusiana na kilimo cha chai.

Thiemo Msemwa ni mkulima mdogo wa chai mkoani Njombe, alikuwa miongoni mwa wahitimu wa mafunzo haya ya mwaka mmoja. Vilevile alipata cheti cha mkulima bora wa chai kutokana na shamba lake kuwa bora.

Nashukuru kupewa cheti cha mkulima bora wa chai. Nimefurahia mafunzo haya ya kilimo endelevu na kanuni kumi za kilimo endelevu. Hata wanangu ninapowaambia waje kwenye shamba la chai wanafurahi kuja shambani kwa sababu kuna mambo mengi ninawafunza,” anasema Msemwa.

Mafunzo hayo yamedhaminiwa na mpango wa Chai Project, kwa lengo la kusaidia viwanda vya chai nchini kwa msaada kutoka The Wood Foundation Africa (TWFA), Gatsby Charitable Foundation (Gatsby) na UKAID.  NOSC imedhamiria kulima chai katika hekta 3,800 na kufikia wakulima 4,000.

Wakulima 4,000 wa chai wanapofikiwa wote ndani ya walau miaka mitano, litakuwa jambo la msingi katika kukuza sekta ya chai.

Kiwanda cha Uniliver kilichopo mkoani Njombe karibu kitakamilika na kitahitaji majani mengi ya chai ambapo malighafi ya kiwanda hicho ni majani ya chai mabichi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles