Na Clara Matimo, Mwanza
Kutokana na sababu mbalimbali zinazosababisha kilimo kutoleta tija kwa wakulima katika halmashauri ya Buchosa mkoani Mwanza baadhi ya wakulima wametaka maafisa ugani kupewa nafasi ya kutoa elimu kuhusu kilimo bora kwenye mikutano ya hadhara ya vijiji.
Pia wameiomba serikali kuwatatulia maafisa ugani changamoto zinazosababisha wasiwafikie kwenye maeneo yao ya kazi na kuwaelimisha kuhusu namna bora ya kuandaa, kulima, kupanda, kuvuna na kuhifadhi mazao yao wanayoyalima ili yakidhi vigezo vya kuuzwa katika masoko ya nje ya nchi.
Wakulima hao wameyasema hayo hivi karibuni wakati wakizungumza kwenye kongamano la uendelezaji sekta ya kilimo katika halmashauri ya Buchosa kupitia mradi wa Tufuatilie kwa Pamoja Rasilimali za Umma, unaotekelezwa na Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na Uchumi wa Nyumbani( TAHEA) kwa ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS) katika Kata za Iligamba, Kazunzu na Nyakalili.
Valeria Ngotezi na Shabani Mussa wakulima kutoka Kata ya Nyakaliro walikiri kwamba serikali inafanya mambo mengi mazuri ili kuwanufaisha wananchi wake katika makundi mbalimbali wakiwemo wakulima lakini baadhi ya watoa huduma wake wamekuwa hawayaelezi vizuri kwa wahusika na kuwapa elimu bora.
“Kwa kweli tumekuwa tukikabiliwa na changamoto ya kuwapata maafisa ugani, huwa tunategemea kwamba wangekuwa wanapewa nafasi ya kutupa elimu kuhusu kilimo bora kwenye mikutano ya hadhara ya vijiji lakini hata wakishiriki kwenye mikutano hiyo wanapewa nafasi ya kutoa tu matangazo lakini sio elimu kuhusu kanuni za kilimo bora,” alisema Mussa na kuongeza:
“Sisi wakulima bila kupewa elimu ya kutosha tusitegemee mafanikio katika sekta ya kilimo ambayo serikali ya awamu ya sita imekiwekea kipaumbele kwa kutaka kila mkulima alime kilimo chenye tija,” alieleza.
Nao wakulima kutoka Kata ya Iligamba, Vedastus Lupilia na Aisha Hassan waliiomba serikali kuwatatulia maafisa ugani changamoto zinazosababisha wasiwafikie kwenye maeneo yao ikiwemo usafiri huku wakikiri kwamba wengi wao kabla ya kupata mafunzo kutoka TAHEA kupitia mradi huo walikuwa hawahudhurii mikutano ya hadhara ya vijiji kwa kuwa hawakutambua umuhimu wake kwamba utawasaidia kupata taarifa sahihi.
“Binafsi naipongeza serikali kwa kuwapa maafisa ugani pikipiki lakini tunapozungumza nao husema kwamba wanashindwa kutufikia kwa sababu wakati mwingine wanakosa mafuta hivyo naiomba serikali iwape motisha hawa maafisa ugani na ihakikishe pikipiki zao zinakuwa na mafuta ili waweze kutufikia mbona kwa walimu wameweza kuwapa wakati hawa nao wanafanya kazi katika idara nyeti, jamani bila chakula kuna mtu anaweza akaendelea kuishi? Alihoji Aisha na kuongeza hawa maafisa ugani wanasimamia sekta nyeti ya wazalishaji chakula,”amesema.
Diwani wa Kata ya Iligamba, Lucas Deus aliishauri Serikali irudishe mashamba darasa na yale ya mfano ili wakulima wapate nafasi ya kwenda kujifunza kanuni za kilimo bora.
“Ukweli ni kwamba wakulima ni wengi lakini maafisa ugani ni wachache hivyo uwepo wa mashamba darasa utasaidia wakulima kulima kilimo chenye tija na kupata mavuno yenye tija,”alisema Deus.
Meneja Mradi wa Tufuatilie kwa Pamoja Rasilimali za Umma kutoka TAHEA, Bundala Ramadhani alisema kongamano hilo limetokana na utafiti uliofanywa na Kamati ya Ufuatiliaji na Uwajibikaji wa Miradi ya Maendeleo katika sekta ya kilimo inayotekelezwa na serikali kwenye Halmashauri ya Buchosa iliyobaini wakulima kutohusika moja kwa moja kwenye kupanga mipango ya kuendeleza sekta hiyo pamoja na bajeti zake.
“Pia watoa huduma nao wanasema hata kama ajenda hiyo itapangwa kwenye mikutano ya hadhara mahudhurio ya wakulima kwenye mikutano ya kupanga bajeti huwa hafifu, kutokana na taarifa hizo TAHEA tukashawishika kupata taarifa kutoka pande zote mbili yaani watoa huduma na wapokea huduma ili kuwajengea uwezo kuhusu wajibu wao,’ alisema Ramadhan.
Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Buchosa, Nestory Mjojo, alisema wananchi wengi wakiitwa kwenye mikutano huwa hawatokei hivyo kukosa fursa ya kupata elimu na taarifa mbalimbali za kisera, sheria na taratibu za Wizara ya Kilimo kuhusu mipango inayoendelea katika kuboresha sekta hiyo.
Hata hivyo kuhusu suala la maafisa ugani kukosa mafuta ya pikipiki ili kuwafikia wakulima na kuwapa elimu ya kanuni za kilimo bora, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam malima Aprili 26,2023 akizungumza kwenye Maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kimkoa wilayani Kwimba mkoani humo aliwaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri zake kuhakikisha wanatoa mafuta kwa maafisa kilimo.
“Mkurugenzi atakayeshindwa kumpa Afisa Kilimo mafuta hatufai, Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametoa pikipiki ili maafisa kilimo na ugani wawafikie wakulima wake na kuwapa elimu jinsi ya kulima kilimo bora chenye tija na nyie maafisa kilimo nikisikia afisa kilimo anatumia pikipiki hizo kama bodaboda nawaonea huruma,”alisema Malima.
Kongamano hilo lililofanyika kwa siku mbili lilikutanisha wadau wa mradi wa Tufuatilie kwa pamoja rasilimali za umma, idara ya kilimo, wakulima maafisa maendeleo ya jamii, Afisa mipango na mhandisi.