ADEN, YEMEN
MHALIFU anayesafirisha wakimbizi kinyume na sheria, amewatupa baharini zaidi ya wakimbizi 120 karibu na fukwe za mji wa Aden nchini Yemen.
Kwa mujibu wa walionusurika, kabla ya hapo jangili huyo aliwagundua watu waliovalia sare, kwa hofu ya kukamatwa akaamua kuwabwaga na kutokomea.
Shirika la kimataifa linalowahudumia wahamiaji – IOM, limesema wakimbizi 29 kutoka Somalia na Ethiopia wamezama na wengine 22 hawajulikani waliko.
Mmoja wa walionusrika alisema kuwa, mhalifu huyo aligeuza njia baadae na kurejea Somalia ili kuwachukua wakimbizi wengine na kuwapeleka katika fukwe za Yemen.
Licha ya vita ya wenyewe kwa wenyewe na kuenea maradhi yanayoambukiza ya kipindupindu nchini Yemen, watu 55,000 wamevuka bahari mwaka huu kutoka pembe ya Afrika na kuingia nchini humo.
Baadhi yao wameelekea katika nchi tajiri za Ghuba kutafuta kazi.