Kulwa Mzee -Dar es salaam
UPANDE wa Jamhuri umewabadilishia mashtaka Wakili Mohammed Majaliwa, Mkurugenzi wa Kampuni ya Jandu Construction & Plumbing Limited, Khairoon Jandu (52), mwanae na mfanyakazi wa benki ambao sasa wanatuhumiwa kughushi sahihi ya marehemu kuiba fedha na kutakatisha zaidi ya Sh bilioni 1.033.
Nyaraka zinazodaiwa kughushiwa ni za mume wa mshtakiwa Khairoon, aliyekuwa mmiliki wa Kampuni ya Jandu Construction and Plumbers Limited iliyopo eneo la Buguruni Kisiwani, Inderjit Sign Jandu ambaye alifariki na kifo chake kiliibua utata na kusababisha ndugu kufungua shauri la kifo cha shaka.
Mashtaka hayo mapya yalisomwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Kassian Matembele na Wakili wa Serikali, Faraja Nguka akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon.
Wakili Nguka aliwataja washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Wakili Majaliwa (39), mfanyakazi wa Benki ya Stanbic, Ibrahim Sangawe (33) na mtoto Zainabu Tharia (26).
Akisoma mashtaka, alidai kati ya Januari na Juni 2020, jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote walitenda kosa la kuongoza genge la uhalifu, kughushi na kuiba.
Inadaiwa kuwa Januari 16 mwaka 2017, jijini Dar es Salaam, washtakiwa Khairoon, Majaliwa na Ibrahim walighushi sahihi ya Inderjit Singh G. Jandu mumewe wa mshtakiwa wa kwanza ambaye ni marehemu, kuonesha ni nyaraka halali ya muhtasari wa kikao cha Kampuni ya Jandu Construction & Plumbing Limited wakati akijua si kweli.
Washtakiwa hao watatu wanadaiwa Mei 24 mwaka 2019 jijini Dar es Salaam walighushi sahihi ya Inderjit Singh G. Jandu kuonesha kwamba mshtakiwa wa kwanza ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo wakati akijua si kweli.
Wakili Nguka alidai washtakiwa hao wanadaiwa Mei 25 mwaka 2019 jijini Dar es Salaam walighushi sahihi ya Inderjit Singh G. Jandu wakionesha kwamba marehemu alihamisha hisa katika kampuni hiyo.
Washtakiwa hao pia wanadaiwa Desemba 18 mwaka 2018, walighushi sahihi wakionesha ni halali imesainiwa na Jandu wakati wakijua si kweli.
Wanakabiliwa pia na mashtaka matatu ya kuwasilisha nyaraka za kughushi Brela.
Shtaka la tisa linawakabili washtakiwa wote, ambao wanadaiwa katika tarehe tofauti mwaka 2020, waliiba Sh 1,033,860,100 mali ya Kampuni ya Jandu Construction & Plumbing Limited.
Kwa upande wa mshtakiwa Ibrahim, inadaiwa kati ya mwaka 2019 na 2020 akiwa mfanyakazi wa Benki ya Stanbic kama meneja, alishindwa kutumia mbinu alizonazo kuzuia utendekaji wa kosa la wizi.
Katika shtaka la kumi, washtakiwa wote wanadaiwa kutakatishaji fedha. Wanadaiwa kwamba katika tarehe zisizofahamika mwaka 2019 jijini Dar es Salaam, walijipatia Sh 1,033,860,100 mali ya Kampuni ya Jandu Construction & Plumbing Limited wakati wakijua ni zao la kosa la wizi.
Washtakiwa hawakutakiwa mujibu lolote na mahakama iliwafahamisha kwamba kesi itakuwa inatajwa kwa njia ya Mahakama Mtandao hadi pale itakapohitajika kufika mahakamani itatolewa hati.
Kesi iliahirishwa hadi Agosti 4 kwa kutajwa.
Awali Wakili Majaliwa na mshtakiwa Ibrahim hawakuwa na makosa ya kutakatisha, lakini mashtaka yote yaliondolewa na kushtakiwa upya.