27.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

Uchaguzi Mkuu sasa kufanyika katikati ya wiki

Nora Damian -Dar es salaam

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema Uchaguzi Mkuu wa Urais, Ubunge na Udiwani utafanyika Oktoba 28, ambayo itakuwa ni siku ya Jumatano tofauti na miaka ya nyuma ambapo ilizoeleka uchaguzi kufanyika Jumapili.

Hivi sasa hekaheka zinaendelea miongoni mwa wanasiasa, vyama vya upinzani na chama tawala CCM kwa michakato ya ndani kwa ajili ya kupata wagombea wa majimbo, udiwani na urais.

Tayari CCM imepata wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Magufuli na urais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi.

Akizungumza jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage, alisema uteuzi wa wagombea wa urais na makamu wa rais, ubunge na udiwani utafanyika Agosti 25.

Aidha alisema kampeni za uchaguzi zitaanza Agosti 26 hadi Oktoba 27. 

Mwanzoni mwa mwaka huu wakati wa mikutano na makundi mbalimbali, viongozi wa dini walipendekeza siku ya kupiga kura iwe ya kazi ili kuwawezesha kuendelea na programu nyingine za ibada.

NEC iliahidi kuwa itazingatia hoja zilizotolewa na wadau na kwamba suala la siku ya kupiga kura wataliangalia kwa macho mazuri.

“Siku ya kupiga kura iwe ya kazi ili viongozi wa dini waendelee na programu za ibada. 

“Hata waumini wengine huwa wanaona kupoteza masaa mawili kwenda kupiga kura atapishana na baraka za Mungu,” alisema Devotha Shimbe wa Kanisa la Waadventista Wasabato.

Tayari tume hiyo imekamilisha uhakiki na uandikishaji wapigakura katika mikoa yote.

Akizungumza hivi karibuni bungeni Dodoma wakati akihitimisha mkutano wa 19 wa Bunge, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema idadi ya wananchi waliojiandikisha kupiga kura imeongezeka ambapo wapigakura halali kwa mwaka huu ni 29,804,992 ikilinganishwa na 23,161,440 wa mwaka 2015.

Kaijage alisema takwimu za awamu ya kwanza na ya pili zinaonyesha kuwa wapigakura wapya walioandikishwa ni 7,326,552, walioboresha taarifa zao ni 3,548,846 na 30,487 wamepoteza sifa.

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa awamu ya kwanza ulianza Julai 18, mwaka jana na kukamilika Februari 23, mwaka huu kwa nchi nzima wakati awamu ya pili ilianza Aprili 17, mwaka huu na kukamilika Mei 5.

Kumbukumbu za mwaka 2015 zinaonyesha wapigakura wanaume walikuwa asilimia 47 na wanawake asilimia 53.

Aidha idadi ya wapigakura vijana waliokuwa na umri wa kati ya miaka 18 na 35 walikuwa asilimia 57 ya wapigakura wote.

Wapigakura waliokuwa na umri wa zaidi ya miaka 50 walikuwa asilimia 18 pekee, huku wengine asilimia 25 wakiwa na umri wa kati ya miaka 36 na 50.

Hata hivyo kati ya wapigakura 23,161,440 waliojiandikisha mwaka 2015, ni 15,589,639 ndio waliopiga kura ambao ni asilimia 67.31 ya wapigakura wote.

Katika uchaguzi huo, Rais Dk. John Magufuli alipata kura 8,882,935 ikiwa ni aslimia 58.46 huku aliyekuwa mpinzani wake kwa wakati huo, Edward Lowassa, akipata kura 6,072,848 ikiwa ni asilimia 39.97 ya kura zote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles