Tunu Nassor, Dar es Salaam
Kwa mara ya kwanza wakazi wa kata ya Bonyokwa Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam leo wameanza kupata huduma ya Majisafi na salama baada ya kukamilika kwa mradi wa kupeleka maji katani hapo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi hao wameshangilia kupata huduma hiyo kutokana na kutokuwa na kuikosa kwa miaka mingi.
Mmoja wa wakazi hao, Saumu Ally amesema kupatikana kwa huduma hiyo kutawasaidia kufanya shughuli zingine za maendeleo baada ya kuwa wanatumia muda mwingi kutafuta maji.
“Tunashukuru sana sasa hata tukioga tutapendeza maana tumekuwa tukinywa maji ya visima ambayo tuliyanunua kwa bei kubwa,” amesema Saumu.
Naye Athanas Masaka amesema ni historia kwa Bonyokwa kushuhudia maji ya Bomba yakitoka katika eneo hilo.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema zaidi ya wateja 1,500 wameunganishiwa huduma hiyo.
“Mradi utawahudumia wakazi 30,00 wa kata hii ambapo tayari mabomba ya inchi 8,4,3, na 2 yamelazwa,” amesema Luhemeja.