25 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 17, 2024

Contact us: [email protected]

Wakazi 4,944 Kwimba kunufaika na huduma ya maji safi

Na Clara Matimo, Kwimba

Zaidi ya wakazi 4,900 wa Kijiji cha Malemve katika Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza watanufaika na huduma ya maji safi na salama kutoka  Ziwa Viktoria hivyo  kumaliza changamoto ya uhaba wa maji iliyokuwepo baada ya mradi uliotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(Ruwasa) kukamilika na kuanza kuhudumia wananchi hao.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima(wa pili kulia) akizindua mradi wa maji Jojiro Malemve uliogharimu zaidi ya Sh milioni 998, (wa kwanza kulia )ni Mwenyekiti wa UWT Mkoa Mwanza Adellah Mayengela.

Mradi huo wa maji wa Jojiro Malemve ambao ulianza kutekelezwa Juni, 2022 na kukamilika Desema 2022 kwa gharama ya zaidi ya  Sh milioni 998 umezinduliwa leo Aprili 26, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima.

Akitoa taarifa ya mradi huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Malima, Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Kwimba, Godliver Gwambasa amesema kukamilika kwa mradi huo kumeongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya hiyo kwa asilimia 1.1 hivyo kufanya upatikanaji wa maji  kufikia asilimia 73 kutoka asilimia 72.

“Chanzo cha maji katika mradi huu ni bomba kuu la KASHWASA, kabla ya mradi huu wananchi wa Kijiji hiki walikuwa wanafuata maji umbali mrefu kutoka kwenye vyanzo ambavyo si salama na uhakika  hivyo kwa sasa utapunguza magonjwa yanayoweza kusababishwa na matumizi ya maji yasiyo safi na salama.

“Pia utawapunguzia  umbali wananchi kutembea muda mrefu kwenda kutafuta maji hivyo watatumia muda mwingi kwenda kwenye shughuli za kiuchumi, kielimu na kijamii,”amesema Godliver.

 Kwa mujibu wa Godliver mradi huo ambao ulikamilika kwa muda uliopangwa umekabidhiwa kwa chombo cha watoa huduma ya maji ngazi ya jamii CBWSO ya Igajo kusimamia shughuli za uendeshaji na matengenezo.

Akizungumza na  mamia ya wananchi wa Kijiji hicho cha Malemve baada ya kuzindua mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima amewataka wananchi kuutunza ili uweza kuwahudumia muda mrefu na wachangie gharama za maji.

“Nimeambiwa kupitia mradi huu mnatozwa Sh 100 kwa ndoo tatu naamini hii gharama ni ya kizalendo kabisa hivyo changieni gharama ili kuweza kuuendesha mradi huu pia mtunze miundombinu yake, mtu anayeharibu miundombinu ya maji napata mashaka ya utanzania wake maana watanzania sisi ni wazalendo,” amesema Malima.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza Adellah Mayengela, amesema kukamilika kwa mradi huo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2020/2025  iliyokusudia  kumtua mama ndoo kichwani ambapo aliwataka watumishi wa umma kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi,  uadilifu na kujituma ili kuwahudumia wananchi kwa wakati.

Awali, akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kimkoa wilayani Kwimba, Mkuu wa Wilaya hiyo Ng’wilabuzu Ludigija alisema  kwa mwaka 2022/2023 serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imepeleka fedha  za maendeleo wilayani humo  Sh bilioni 19 na miradi mbalimbali ya maendeleo inaendelea kutekelezwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles