29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Wakazi 23,000 kunufaika na mradi wa maji wa WaterAid Halmashauri ya Arusha

Janeth Mushi, Arusha
 
Zaidi ya wakazi 23,000 wanaoishi katika vijiji vitano vilivyopo katika Halmashauri ya Arusha, wameondokana na adha ya matumizi ya maji yenye kiasi kikubwa cha madini ya Flouride baada ya kukamilika kwa mradi wa maji safi na salama.

Mradi huo ulikuwa umetekelezwa na Shirika la Kimataifa la WaterAid Tanzania, kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza,umegharimu Sh bilioni 11 ambapo jana umekabidhiwa kwa Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA) kwa ajili ya usimamizi.

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Wizara ya Maji, Simon Nkanyemka.

Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa mradi huo baada ya kukamilika kwa asilimia 100, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Olkokola,Kata ya Lemanyata,wameshukuru wadau hao kwa kutekeleza mradi huo kwani kipindi cha nyuma walikuwa wakiteseka na maji yenye Flouride.

Mmoja wa wananchi hao, Judica Philemon, amesema wanawake na watoto walikuwa wahanga wa tatizo la maji na kuwa baada ya kukamilika kwa mradi huo kumewasaidia kuondokana na madhara yatokanayo na maji ya flouride ikiwemo kupinda miguu,migongo pamoja na kuharibika meno.

“Kipindi cha nyuma tulikuwa tunateseka kwa kukosa huduma ya maji safi na salama,watoto walikuwa wanaenda shule wakiwa wachafu,kuna watu walikuwa wakienda kutembelea watoto wetu shulemi wanasema hatuwatunzi ila siyo kwamba tulikuwa hatuwatunzi,ilikuwa ni shida ya maji.

“Walikuwa wanaenda shule wakati mwingine bila kunawa hata uso ila kwa sasa wanaenda wakiwa wasafi na maji haya yatasaidia kwani yale ya mwanzo yameleta athari kwa jamii ikiwemo kuharibika mifupa na meno,” amesema Judica.

Akizungumza kwa niaba ya wazee wa mila wa kijiji hicho, Reuben Ole Sikorei amesema wanashukuru kwa kuwepo kwa mrad huo na kuwa watahakksha wanausimamia usharibiwe ili uweze kuwanufaisha kwa kipindi kirefu.

“Tunashukuru kwa uwepo wa mradi huu na tulianza kuulinda kuanzia wakati wa ujenzi usiku na mchana hasa baada ya kubaini ni kwa manufaa yetu ila tunaomba utaratibu wa kulipia maji kabla uwekwe sawa kwani huku kijijini ni mtu mmoja tu ndiyo anatuuzia token za maji,” amesema Sikorei.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la WaterAid Tanzania, Anna Mzinga, amesema mradi huo mpaka sasa umefikia wananchi zaidi ya 23,000 kati ya wanufaika 50,000 wanaotarajiwa kunufaika na mradi huo ifikapo mwaka 2030.

“Toka kuanzishwa kwa utekelezaji wa mradi huu mwaka 2017 hadi leo tunapowakabidhi AUWSA, mradi huu una thamani ya Sh bilioni 11, ambapo Sh bilioni 10.5 ni ufadhili kutoka Serikali ya Uingereza kupitia Idara ya Maendeleo na Sh milioni 500 ni kutoka WaterAid kama sehemu ya mchango wetu kwa jamii.

“Leo ni furaha kwetu sote kukabidhi mradi huu kwa bijiji hivi tukiamini kabisa wataendeleza malengo ya mradi huu na tunatumaini watahakikisha usimamizi thabiti wa vituo vya maji pamoja na teknoojia ya kuhuisha kwa muda mrefu kwa kadri itakavyowezekana,” amesema Anna.

Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Wizara ya Maji, Simon Nkanyemka amesema ni wakati wa taasisi mbalimbali zinazotarajia kutengeneza miradi kuiga mfano wa mradi huo ikiwemo teknolojia iliyotumika ya kuondoa flouride ya kwenye maji.

“Katika Wizara ya Maji kwa sababu tunataka mwananchi agharamie uendeshaji wa miradi, tunahimiza sana utumiaji wa teknolojia ambayo inapunguza gharama za uendeshaji, teknolojia ya malipo ya maji kabla inasaidia kuhakikisha makusanyo yanakusanywa kwa wakati na usahihi.

“AUWSA kuna usemi unasema ukishikwa shikamana, pamoja na misaada wanayotupa wenzetu wa kuwekeza na sisi tuhakikishe tunaweka mipango thabiti ya kuhakikisha tunafikisha maji katika vijiji vya jirani ambayo vimepangwa kupata huduma za maji,” amesema Nkanyemka.
 
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arusha, Saad Mtambule amevitaja vijiji hivyo ni Lengijave, Olkokola, Seuri, Ngaramtoni na Ekenywa na kuwa upatikanaji wa mradi huo una manufaa makubwa kwa wananchi hao kiafya na kiuchumi.

Amesema awali maji hayo yalikuwa na kiwango kikubwa cha madini hayo ya Flouride ambapo ilikuwa miligramu 12 kwa lita moja huku viwnago vya kimataifa vikitaka iwe miligramu 1.5 kwa lita moja na kuwa athari zake kiafya ni kubwa katika eneo hilo.

“Tunashukuru wadau mbalimbali mlioshirikiana na sisi katika kutekeleza mradi huu kwani awali ulikuwa na changamoto ikiwemo wingi wa flouride hivyo tunashukuru kwenye designing walianza kupitia upya na kuingiza components ambazo zinasaidia kupunguza floride na maji kuwa safi na salama baada ya kuchujwa,” amesema.

Amesema kabla ya mradi katika kijiji cha Olkokola,upatikanaji wa maji ulikuwa asilimia kati ya 45 hadi 52 ila kwa sasa wanafikia asilimia 72 ya upatikanaji wa maji safi na salama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles