Aziza Masoud na JONAS MUSHI-DAR ES SALAAM
SERIKALI imetoa agizo kwa taasisi zake kutumia Wakala wa Majengo (TBA) kwa ujenzi wa majengo yake na si vinginevyo.
Tangu utawala wa Rais Dk. John Magufuli uingie madarakani, umependelea zaidi kufanya shughuli zake kwa kutumia taasisi zake, na si kampuni za watu binafsi.
Tayari TBA imeshapewa miradi mikubwa ya ujenzi, ikiwamo ujenzi wa nyumba za makazi za Magomeni Kota zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi Bunju na ule wa hosteli za kulala wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Tamisemi kupitia barua yake ya Septemba 29, mwaka huu ambayo MTANZANIA Jumapili imeiona ikiwa imesainiwa na Katibu Mkuu wake, Mhandisi Mussa Iyombe, imetoa maagizo kwa makatibu tawala wa mikoa kuhakikisha ujenzi wowote wa nyumba za halmashauri unafanywa na TBA.
“Nimepokea maelekezo kuwa ujenzi wa majengo yote ya Serikali yanayohusisha nyumba za makatibu tawala wa mikoa, makatibu tawala wa wilaya pamoja na ujenzi wa ofisi za halmashauri mpya, ufanywe na TBA na si vinginevyo,” aliagiza Iyombe kupitia barua hiyo yenye kumbukumbu namba AB 39/156/01E/178.
Barua hiyo inaendelea kuagiza kuwa Ofisi ya Rais Tamisemi kwa kushirikiana na TBA inafanya utaratibu wa kufufua mkataba unaohusu majengo hayo ili kazi ziendelee.
“Hivyo mnaelekezwa kuzingatia maelekezo haya na kuziagiza halmashauri katika mikoa yenu kufuata maelekezo hayo pindi zinapofanya mchakato wa ujenzi wa ofisi zao,” ilisema barua hiyo.
Mmoja wa maofisa waandamizi wa Tamisemi aliyezungumza kwa simu na MTANZANIA Jumapili, kwa masharti ya jina lake kutoandikwa gazetini, alisema agizo hilo limetolewa katika halmashauri zote nchini.
Maagizo ya Tamisemi yanaonyesha kutimiza azma ya Rais Magufuli ya kutaka ujenzi wa nyumba na majengo ya taasisi za Serikali kujengwa na TBA au Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Mara kadhaa Rais Magufuli amekuwa akitoa kauli za kuisifia TBA kutokana na kujenga nyumba kwa gharama nafuu na kuahidi kuipa miradi mingi zaidi.
Katika moja ya hotuba zake alizozitoa Septemba, mwaka huu, Rais Magufuli alinukuliwa akisema Serikali ilivyotangaza zabuni ya mradi wa hosteli za wanafunzi wa UDSM zilizopo eneo la Mlimani, kampuni binafsi za wakandarasi zilijitokeza na kutaka kuzijenga kwa gharama ya kati ya Sh bilioni 50 hadi 100, lakini sasa hivi zinajengwa na TBA kwa gharama ya Sh bilioni 10 tu wakishirikiana na vijana Watanzania.
Ujenzi wa hosteli hizo zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 3,840 ulizinduliwa mwanzoni mwa Septemba, mwaka huu na unatarajiwa kumalizika mwakani.