27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wajasiriamali wanawake kukopeshwa hadi Shilingi bilioni 3

Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Wanawake wajasiriamali nchini wana fursa ya kukopa kuanzia Sh milioni 200 hadi Sh bilioni 3 katika Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB) ili kuwawezesha kukuza biashara zao na kuweza kushindana kwenye masoko ya ndani na nje.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 5, 2024 na Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Biashara kutoka TIB, Joseph Chilambo wakati wa warsha maalumu iliyoandaliwa na Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) ikiwakutanisha wanawake wajasiriamali na wadau tofauti.

Akizungumza kwenye warsha hiyo, Chilambo amesema taasisi yake inafurahi kupata fursa ya kukutana na wanawake hao ili kuwaeleza fursa ambazo TIB wanazitoa kwa ajili yao kupitia bishara wanazizifanya.

Amesema wanatambua kwamba wanawake ni kundi linalopitia changamoto nyingi kwenye biashara kama vile

“Mpaka sasa benki ina mpango maalumu ambao inautekeleza wa kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kwa sababu tumeona hawa wana changamoto kubwa sana ya kupata mikopo maeneo mbalimbali.

“Kuna mahitaji ya vitu kama nyaraka, dhamana na vinginevyo vinavyowatatiza, lakini sisi kama Benki ya Maendeleo tumeamua kuondoa changamoto hizo na tuna fursa ya kukopa kuanzia Sh milioni 200 hadi Sh bilioni 3 kwa ajili ya uwekezaji.

“Sisi kazi yetu kubwa ni uwekezaji, wale wanaotaka kufungua viwanda vyao, benki yetu inaweza kuwapatia mikopo ili kuanzisha hivyo viwanda au kuvikuza ili viwe vikubwa zaidi,” amesema Chilambo.

Akizungumzia vigezo vya kupata mikopo hiyo, mkurugenzi huyo amesema sifa ya kwanza ni kuwa na biashara iliyosajiliwa na wanawashauri wasajili biashara zao kama kampuni binafsi, hivyo wanakuwa na hati ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela).

Pili, amesema lazima wafanyabiashara wawe na mpango wa biashara ambao umeandikiwa. Amesema katika kurejesha mkopo, wanaangalia na aina ya biashara ili waweze kukadiria marejesho kulingana na mkopo wenyewe na ukubwa wa biashara.

“Benki imetenga Sh bilioni 30 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati. Na hicho ni kiasi cha kuanzia, siku za nyuma hatukuwa na huduma kama hiyo. Kadiri mafanikio yanavyopatikana, tunaweza kuongeza,” amesema.

Kwa upande wake, Rais wa TWCC, Mercy Sila amewahimiza wanawake kuchukua mikopo ya benki kwa ajili ya kukuza biashara zao na kuachana na dhana ya kuogopa riba ndogo zinazowekwa kwenye mikopo hiyo.

“Tuchangamkie fursa ya mikopo, tusiogope. Tuna mabenki mengi yanatoa mikopo kwa wajasiriamali. Kwenye halmashauri kule kuna mikopo ya asilimia 10 kwa ajili ya wanawake, vijana na wenye ulemavu,” amesema.

Sila amewahimiza wanawake wafanyabiashara kushindania zabuni za Serikali ili watoe huduma kwa sababu huko kuna fursa kubwa ukizingatia kwamba Sheria ya Manunuzi ya Umma inaelekeza kwamba asilimia 30 ya matumizi ya Serikali yaende kwa makundi maalumu.

Mmoja wa wajasiriamali walioshiriki warsha hiyo, Tabitha Luwanga amesema tangu amejiunga na TWCC, biashara yake ya kuzalisha na kuuza vidani (culture) kwa ajili ya urembo umekua na soko lake pia limeongezeka.

“TWCC imenisaidia sana, imenikutanisha na watu tofauti na pia nimejifunza namna ya kufanya biashara kisasa na kujua taratibu zote za usajili na kikodi. Tofauti kubwa ninaiona kati ya sasa na zamani, nimepiga hatua kubwa mbele,” amesema mjasiriamali huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles